Rais wa Ukraine Volodymyr Zelenskyy amehimiza mataifa ya bara Ulaya yaliyo na urafiki na Ukraine kuwapa zana za vita kwa ajili ya kujilinda.

Rais huyo anadai kuwa gharama ya amani na usalama ni ghali akiwataka maswahiba wao kujitokeza katika wakati huu mgumu katika mikono ya watesi wao.

Kwa mujibu wa Zelenskyy, vita hivyo si vya Ukraine pekee, bali ni vya bara Ulaya kwani uhuru kwa bara hilo unatishiwa na Urusi na huenda mataifa mengine pia yakashambuliwa.

“Haya ndiyo waliyo nayo wandani wetu. Hivi ndivo vilvyofunikwa na vumbi katika sehemu zao za kuvihifhadhi. Hivi vita sio tu kwa usalama uhuru wa Ukraine bali uhuru wa bara Ulaya kwa jumla. Kwa sababu mataifa mengine kama vile Poland, Slovakia na Ulaya ya Magharibi yamo katika hatari ya kushambuliwa na Urusi,” alisema kupitia kwa kanda ya video.

Zelenskyy sasa anawataka wandani wao kuwapa angalau asilimia moja ya vifaa vyote vya NATO kama vile ndege za kivita, matenki na silaha zingine.

“Asilimia moja tu. Hatujaomba zaidi ya hapo. Na hatutaomba zaidi ya hapo. Tumekuwa tukisubiri kwa siku 31,” alisema.

Rais huyu alisisitza kuwa washirika wao wanahijtajika kujitokeza na kusaidia Ukraine akitoa shukrani kwa wote waliojitoa mhanga kuilinda Ukraine.

Zelenskyy alishukuru jeshi la Ukraine na vikosi vingine vya usalama kwa kusimama tisti dhidi ya mashambulizi kwa zaidi ya mwezi mmoja sasa.

Dkt Mpango kumuwakilisha Rais Samia UAE
Rais Kenyatta: DP Rutto alitaka kuning'oa madarakani