Kocha Mkuu wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC Franco Pablo Martin amemuondoa Kiungo Mshambuliaji Hassan Dilunga kwenye mipango yake kwa msimu huu 2021/22.

Dilunga alipata majeraha ya goti Februari 9, mwaka huu akiwa mazoezini na kikosi cha Simba kilichokuwa kikijiandaa na mchezo wao wa kwanza wa hatua ya makundi Kombe la Shirikisho Afrika dhidi ya ASEC Mimosas ya Ivory Coast.

Kocha Pablo amesema amefanya maamuzi ya kumuondoa Dilunga kwenye mipango yake ili kutoa nafasi ya kuendelea na matibabu.

Amesema hakutarajia kama kiungo huyo angekaa nje ya Uwanja kwa muda mrefu, lakini kilichotokea hana budi kukubaliana nacho na kumpa muda wakuendelea kupata matibabu.

“Kuhusiana na Dilunga mwanzo hatukudhani angekuwa na jeraha kubwa ambalo lingemuweka nje ya uwanja kwa muda mrefu.

“Lakini kwa bahati mbaya tunaweza kumkosa labda mpaka mwishoni mwa msimu, hivyo tunalazimika kumuondoa kwenye mipango yetu kwa sasa mpaka pale taarifa za timu yetu ya madaktari itakapoonyesha kuwa yupo tayari kujiunga na timu.” amesema Kocha Pablo

Nyota huyo ndiye mchezaji pekee wa Simba SC ambaye ni majeruhi kwa sasa, ambapo kutokana na jeraha hilo amekosekana kwenye michezo sita ya michuano ya Kombe la Shirikisho, Ligi Kuu Tanzania Bara na Kombe la Shirikisho ‘ASFC’.

Simba SC tayari imeshaanza maandalizi ya kujiandaa na mchezo wa Mzunguuko wa sita wa ‘Kundi D’ Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya USGN ya Niger.

Simba SC itakua mwenyeji wa mchezo huo, utakaopigwa Jumapili (April 03), Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikihitaji alama tatu muhimu zitakazoipeleka Robo Fainali.

Sky Sports: Abramovic yupo sawa
Haji Manara: Fiston Mayele hauzwi