Mashabiki na Wanachama wa Klabu ya Simba wameombwa kuwa watulivu katika kipindi hiki ambacho klabu yao inahusishwa na mpango wa kumsajili Mshambuliaji kutoka Niger Victorien Adebayor.

Simba SC kwa zaidi ya mwezi mmoja imekua ikitajwa kumuwania Mshambuliaji huyo, baada ya baadhi ya viongozi wake kuridhishwa na uwezo wake tangu timu yao ilipokutana na USGN katika mchezo wa Kombe la Shirikisho Barani Afrika mjini Niamey-Niger.

Meneja wa Habari na Mawasilino wa Simba SC Ahmed Ally amesema bado ni mapema mno kwa klabu hiyo kusema lolote kuhusu usajili wa Adebayor, hivyo Mashabiki na Wanachama wanapaswa kutulia na kuendelea kuipa nguvu timu yao kwenye Michuano ya ndani na nje ya Tanzania.

Amesema endapo Mshambuliaji huyo atasajiliwa Simba SC, kila kitu kitaanikwa hadharani na kama itawezekana kwa Mashabiki na Wanachama kwenda Uwanja wa Ndege kumpokea watafanya hivyo, lakini kwa sasa ni muda wa kuipa nguvu timu yao.

“Muda utaongea, wasiwe na mashaka hata kidogo, kama Mshambuliaji huyu anakuja Msimbazi, Mashabiki na Wanachama wataambiwa na wakipenda watakwenda Uwanja wa Ndege kumpokea, kama hatakuja Msimbazi pia wataambiwa.”

“Kwa hiyo ningependa kuwaambia Wanasimba wote Muda utasema ukweli kuhusu jambo la usajili wa huyu mchezaji, kwa sasa tuendelee kuiunga mkono timu yetu, ina majukumu ya kutetea Ubingwa na kuliwakilisha Taifa Kimataifa.” Amesema Ahmed Ally

Hadi sasa Adebayor ndio mchezaji pekee aliyefunga mabao mengi zaidi kwenye Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, licha ya klabu yake USGN kuondolewa kwa kushika nafasi ya mwisho katika msimamo wa Kundi D.

Adebayor ambaye alikua sehemu ya kikosi cha USGN kilichoikabili Simba SC Jumapili (April 03) katika Uwanja wa Benjamin Mkapa Jijini Dar es salaam amefunga mabao 06.

Ajibu aitumia salamu Young Africans
Juventus yajiondoa mbio za ubingwa Italia