Kiungo Mshambuliaji wa Azam FC Ibrahim Ajibu amewataka Young Africans kujiandaa kwa kipigo kesho Jumatano (April 06), watakapokutana kwenye mchezo wa Mzunguuko wa 19 wa Ligi Kuu Tanzania Bara.

Azam FC itakua nyumbani Azam Complex, Chamazi jijini Dar es salaam, kuikaribisha Young Africans ambayo mpaka sasa haijapoteza mchezo tangu ilipoanza msimu huu 2021/22.

Ajibu amesema Azam FC imejiandaa kikamilifu kuelekea mchezo huo, huku wakitarajia kupambana na kupata ushindi katika Uwanja wao wa nyumbani, ili kulipa kisasi cha kufungwa mabao 2-0 walipokutana na Young Africans Uwanja wa Benjamin Mkapa katika Duru la Kwanza la Ligi Kuu msimu huu.

Hata Hivyo Kiungo huyo wa zamani wa Simba SC, amekiri wazi kuwa Young Africans ina kikosi kizuri na imara, lakini bado anaamini Azam FC ina kikosi imara zaidi na nsio maana hana shaka na alama tatu za kesho Jumatano (April 06).

“Tunajua kama Young Africans ni timu nzuri na inaongoza msimamo wa ligi, lakini tumejipanga kukabiliana nayo na kuchukua alama zote tatu,” amesema Ajibu ambaye pia amewahi kuichezea Young Africans.

Young Africans inaongoza msimamo wa Ligi Kuu ikiwa na alama 48 baada ya michezo 18 huku Azam FC ikishika nafasi ya tatu kwa kumiliki alama zake 28, saba nyuma ya Simba SC iliyopo nafasi ya pili.

Bumbuli: Azam FC watatuchangia alama sita
Usajili wa Adebayor Simba SC, Mashabiki wapewa ujumbe