Beki wa Kati kutoka nchini Kenya na klabu ya Simba SC Joash Onyango Achieng ataukosa mchezo wa kwanza wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini, kufuatia kadi tatu za njano alizozipata kwenye michezo ya Kundi D.

Onyango alikua na kadi mbili za njano kabla ya mchezo wa mwisho wa Kundi D dhidi ya USGN ya Niger, uliopigwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, Jumapili (April 03).

Beki huyo alionyeshwa kadi ya tatu katika mchezo huo uliomalizika kwa Simba SC kuibuka mbabe kwa mabao 4-0, baada ya kumchezea hovyo Mshambuliaji wa USGN Victorien Adebayor.

Kwa mantiki hiyo Benchi la Ufundi la Simba SC litakua na jukumu la kumtumia Beki kutoka nchini Ivory Coast Pascal Wawa au Beki mzawa Kennedy Juma ili asaidiane na Beki Hennock Inonga kwenye mchezo huo ambao umepangwa kuchezwa kati ya April 15-17.

Hata hivyo Onyango atakua na nafasi ya kurejea kikosini kwenye mchezo wa mkondo wa pili, ambao utapigwa Afrika Kusini kati ya April 22-24.

Naye kiungo kutoka nchini Mali Sadio Kanoute ataukosa mchezo wa Mkondo wa kwanza dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika kufuatia kuwa na kadi tatu za njano.

Wizkid aonesha ukomavu wa kiushindani
Chama awabwaga Mayele, Lusajo Ligi Kuu