Wizara ya Afya nchini Kenya imefichua kuwa angalau wasichana 98 kati ya umri wa miaka 10 na 19 waliambukizwa virusi vya ukimwi kila wiki kati ya Januari na Februari.
Kwa mujibu wa Katibu katika Wizara ya Afya Susan Mochache, Kenya vilevile ilirekodi visa 45,724 vya mimba kwa wasichana wa umri wa kati ya miaka 13 na 19 huku visa vya dhulma za kijinsia 2,196 vikiripotiwa kwa wasichana wa umri wa kati ya miaka 12 na 17.
Mochache alizungumza manna hayo akiwa eneo la Pwani katika mkutano wa kitaifa wa siku nne na makamishna wa kaunti kuhusu wajibu wao katika kukabili virusi vya HIV, mimba za mapema na dhulma za kijinsia.
Mochache amesema kuwa kumekuwa na juhudi kubwa za kumaliza majanga hayo matatu ambayo yameendelea kuwakandamiza watoto wa kike nchini humo.
Katibu huyo aliendelea kwa kusema kuwa kati ya mwaka 2013 na 2021, juhudi za kudhibiti HIV zilipunguza vifo kutokana na ugonjwa wa ukimwi kwa asimilia 67.
Hata hivyo, Mochache alielezea wasiwasi wake na visa vingi vya dhulma za kingono na kijinsia ambazo zimewaacha wanawake na wasichana wengi wakiwa na virusi vya HIV kando na kuwapokonya hadhi yao.
Amesema matukio 12,520 vya dhulma za kingono na kijinsia viliripotiwa nchini mwaka jana.