Uongozi wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC umetoa shukurani kwa Mashabiki na Wanachama wake, kufuatia kuitikia wito wa kufika Uwanja wa Benjamin Mkapa kuishangilia timu yao ilipokua ikicheza dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini.
Jana Jumapili (April 17) Simba SC ilikua mwenyeji wa Orlando Pirates katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, ikianza kampeni za kusaka tiketi ya kucheza Nusu Fainali Kombe la Shirikisho kwenye mchezo wa Mkondo wa Kwanza wa Robo Fainali.
Shukran za Simba SC kwa Wanachama na Mashabiki zimetolewa na Meneja wa Habari na Mawasiliano wa klabu hiyo Ahmed Ally kwa kuandika ujumbe mzito katika ukurasa wake wa Instagram.
Ahmed aandika: TUMEWAITA MKAITIKAAA
Ninyi ni watu bora sana ??
Sisi tunajivunia nyie??
Ninyi ni mashabiki wenye kujua mpira na mashabiki wenye mapenzi ya kweli na timu yenu
Kuna watu wamefuturu saaa 4 baada ya mechi wamekubali kukaaa njaa muda wote huo kwa sababu ya timu yao
Niwahakikishie tutaendelea kutengeneza timu bora Ili muendelee kupata burudani.
Ahmed Ally kwa juma zima aliendesha Kampeni ya Hamasa kwa Wanachama na Mashabiki wa Klabu ya Simba SC katika baadhi ya maeneo ya Jiji la Dar es salaam.
Ahmed akishirikiana na baadhi ya Viongozi na Wanachama wakongwe wa Simba SC walizindua Kampeni hiyo Jumanne (April 12) kwenye Tawi la Tunawakera lililopo eneo la Maduka Mawili, Chang’ombe-Temeke.
Siku zilizofuata aliendesha kamepni hiyo eneo la Feri hadi Kigamboni, Chuo Kikuu cha Dar es salaam, Temeke, Mbagala, Chamazi hadi Chanika.
Simba SC ilichomoza na ushindi wa 1-0 dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini jana Jumapili (April 17), na sasa inasubiri mchezo wa Mkondo wa pili utakaorindika Jumapili (April 24) Afrika Kusini.
Simba SC italazimika kulinda ushindi wake wa 1-0, ama kusaka ushindi zaidi katika mchezo wa Mkondo wa pili ugenini, ili kupata tiketi ya kutinga Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.
Kwa upande wa Orlando Pirates italazimika kusaka ushindi wa mabao mawili kwa sifuri na kuelendelea, ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.