Kocha wa Orlando Pirates Mandla Ncikazi anaamini Simba SC haikushinda kihalali katika mchezo wa Mkondo wa kwanza Hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Simba SC ilichomoza na ushindi wa bao 1-0, jana Jumapili (April 17), Uwanja wa Benjamin Mkapa, huku ikitarajia kucheza mchezo wa Mkondo wa pili Jumapili (April 24) nchini Afrika Kusini, ili kujua hatma ya kutinga Nusu Fainali.

Kocha Mandla Ncikazi amesema kwa uhakika kuwa Simba SC haikustahili kushinda mchezo huo, alipozungumza na Waandishi wa Habari baada ya dakika 90 kumalizika Kwa Mkapa.

Kocha Mandla Ncikazi alisema: “Media zenu zote hapa zinaenda kudanganya na kuandika uongo, semeni ukweli, Simba hakustahili kushinda, Simba wamebebwa, hawajatutreat vizuri tangu tumefika, penati waliyopewa hawakustahili, VAR imewekwa lakini haijatumika katika maamuzi”

“Kwa nini mnafanya haya kwa Waafrica wenzenu ? Je tutainua soka la Africa kwa namna hii ?! Na tunatoka hapa tukijisifu Simba kashinda, Simba hawajashinda referee ndiye amefanya Simba washinde, Kama kweli Simba ni mabingwa wa kuhonga katika soka, ikibainika wanahonga mpaka waendesha (VAR) tutafika (CAF), mpaka (FIFA) tena wanaweza fungiwa mechi za Confederations of African Football (CAF)”

“Mliyotufanyia hapa kuanzia Airport, Stadium hadi hotelini, Je mtafurahi tukiwafanyia haya pia mkija South Africa ? Tunarejea nyumbani kujipanga sisi hatutalipiza”

Simba SC italazimika kulinda ushindi wake wa 1-0, ama kusaka ushindi zaidi katika mchezo wa Mkondo wa pili ugenini Afrika Kusini siku ya Jumapili (April 24), ili kupata tiketi ya kutinga Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Kwa upande wa Orlando Pirates italazimika kusaka ushindi wa mabao mawili kwa sifuri na kuelendelea, ili kujihakikishia nafasi ya kucheza Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika.

Rayvanny kaipiga chini WCB?
Dkt.Kijaji: Anayekwamisha utalii na uwekezaji, atakuwa mfano