Mshambuliaji wa zamani wa Simba SC Dua Said ameshindwa kutabiri nani ataibuka na alama tatu katika mchezo wa Ligi Kuu Tanzania Bara ambao utazikutanisha klabu kongwe katika Soka la Bongo, Uwanja wa Benjamin mkapa jijini Dar es salaam.

Young Africans ambayo msimu huu imeonyesha kuwa na umahiri mkubwa wa kikosi huku ikiwa haijapoteza mchezo, itakutana na Simba SC inayotetea taji la Ligi Kuu Tanzania Bara kwa mara ya tano mfululizo.

Dua Said amesema mchezo huo unatarajiwa kuwa na ushindani mkubwa uliojaa ufundi wa hali ya juu, kutokana na vikosi vya timu zote mbili ambavyo kwa hivi karibuni vimeonyesha kuwa katika hali nzuri.

Amesema Simba SC ambayo imetoka kupoteza mchezo dhidi ya Orlando Pirates ya Afrika Kusini itahitaji kuendeleza mazuri iliyoyafanya kwenye Michuano ya Kimataifa ambapo kwa msimu huu imeishia hatua ya Robo Fainali, huku Young Africans nayo itahitaji kuendeleza rekodi ya kucheza soka ambalo limeifanya timu hiyo kuwa na msimu mzuri hadi sasa.

“Simba wametoka kupoteza katika Michuano ya Kimataifa na Young Africans inahitaji Ubingwa kwa kuhakikisha inaifunga Simba SC, kwa hiyo hii Dabi mimi ninaiona itakua ngumu na itajaa ufundi mwingi sana.”

“Naamini Simba SC haitakubali kufungwa na Young Africans katika mchezo wa Jumamosi ili iwe mgogo kwa wapinznai wao kutangaza ubingwa msimu huu, na Young Africans hawatakua tayari kupoteza dhidi ya Simba SC ili kuendeleza rekodi ya kutokufungwa msimu huu, kwa hiyo nikitazama bado naona mambo ni mgumu na kutabiri huu mchezo ni mtihani mkubwa.” Amesema Dua Said

Simba SC inakwenda kukutana na Young Africans huku ikiwa na asilimia kubwa ya kuutema ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu, kufuatia kuachwa kwa alama 13 katika msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa, huku timu hiyo ikicheza michezo 19.

Young Africans iliyocheza michezo 20 inaongoza msimamo ikiwa na alama 54, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 41, huku Namungo FC ikiwa nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 29 na Azam FC ipo nafasi ya nne kwa kumiliki alama 28.

SIMULIZI :Video za ngono zilivyomponza bosi wangu
Hassan Bumbuli: Hata tukipoteza tutaendelea kuwa na furaha