Meneja wa Habari na Mawasilino wa Klabu Bingwa Tanzania Bara Simba SC Ahmed Ally amesema anaamini Mashabiki na Wanachama wa klabu hiyo watafuta machozi na kumaliza Manung’uniko ya kupoteza mchezo wa Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates, baada ya kikosi chao kukusanya alama tatu za mpambano wa Jumamosi (April 30), dhidi ya Young Africans.

Simba SC itakua mgeni wa Young Africans Uwanja wa Benjamin Mkapa, baada ya kurejea nchini juzi Jumatatu (April 28), ikitokea Afrika Kusini ilipokua na jukumu la kusaka tiketi ya kucheza Nusu Fainali ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika dhidi ya Orlando Pirates, lakini ilitolewa kwa mikwaju ya Penati 4-3.

Ahmed Ally amesema kikosi chao kinaendelea na maandalizi ya mchezo huo unaosubiriwa kwa hamu kubwa, na kila mmoja ndani ya Simba SC anaamini wanakwenda kupambana kwa lengo la kuzipata alama tatu sambmaba na kuwa timu ya kwanza kuifunga Young Africans msimu huu 2021/22.

Amesema wachezaji wao wote wana nia ya kuwafuta machozi Mashabiki na wanachama walionyesha kuwa pamoja na timu yao wakati wote msimu huu 2021/22, hivyo ni jukumu lao kuhakikisha wanatimiza wanachokikusudia Jumamosi (April 30).

“Tayari tumeshaanza kambi ya kujiandaa na mchezo wetu dhidi ya Young Africans utakaopigwa Jumamosi, tunaamini utakua mchezo muhimu kwa pande zote mbili, lakini kwetu utakua mchezo ambao utawafariji Mashabiki na Wanachama wetu ambao walipoteza tabasamu lao baada ya kutolewa kwa penati na Orlando Pirates Jumapili (April 24).”

“Kwa kuzingatia umuhimu wa mchezo huu, Benchi la Ufundi liliona kuna ulazima wachezaji kuanza kambi moja kwa moja baada ya kuwasili Dar es salaam tukitokea Afrika Kusini na hilo limefanikiwa kwa kiasi kikubwa, kwa sababu wachezaji wote wameonesha kuwa katika morari ya hali ya juu kwa kukubali hilo kwa maamuzi ya pamoja.”

“Sisi ndio timu yenye mashabiki bora Tanzania na hilo halina ubishi, hivyo Mashabiki na Wanachama wanapaswa kuja kwa wingi uwanjani ili kuishangilia timu yao ambayo ina dhamira ya kurejehsea tabasamu la furaha kwa kuifunga timu inayojifanya msimu huu haijafungwa.” Amesema Ahmed Ally.

Simba SC inakwenda kukutana na Young Africans huku ikiwa na asilimia kubwa ya kuutema ubingwa wa Tanzania Bara msimu huu, kufuatia kuachwa kwa alama 13 katika msimamo wa Ligi Kuu hadi sasa, huku timu hiyo ikicheza michezo 19.

Young Africans iliyocheza michezo 20 inaongoza msimamo ikiwa na alama 54, ikifuatiwa na Simba SC yenye alama 41, huku Namungo FC ikiwa nafasi ya tatu kwa kufikisha alama 29 na Azam FC ipo nafasi ya nne kwa kumiliki alama 28.

Gesi ya Urusi yasitishwa Poland, Bulgaria
Dkt.Slaa ataka Taarifa ya CAG isijadiliwe, amkosoa Zitto