Swaum Katambo – Katavi.

Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika imetoa eneo lenye ukubwa wa ekari zaidi ya 438 kwa ajili ya kuwapatia wahanga wa mafuriko waliopo katika mwambao wa ziwa Tanganyika na maeneo jirani.

Hayo yamesemwa na Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Wilaya hiyo, Halima Kitumba katika zoezi la utoaji misaada kwa wahanga wa mafuriko katika Kijiji cha Ikaka B na maeneo mengine ambapo amesema ekari hizo zenye thamani ya shilingi milioni 64 tayari zimebainishwa.

Amesema, Kamati ya maafa Wilaya imepokea na kufanya tathmini ya kina na mahitaji muhimu kwa wahanga wa mafuriko katika mwambao wa ziwa Tanganyika na kubaini mahitaji makuu matatu yaliyo athiriwa zaidi ikiwemo kuwaondoa wananchi wanaoishi kwenye mikondo ya maji kwa kuwapatia viwanja, miundombinu ya barabara mpya na umeme ambayo itagharimu kiasi cha shilingi za kitanzania zaidi ya bil 1.625.

Halima ameongeza kuwa, kabla ya misaada waliyopatiwa wahanga, tathmini ilionyesha mahitaji ya kibinadamu yaliyokuwa yanahitajika ya zaidi ya shilingi milioni 100 ambapo kwa kuanza wamewapatia wahanga magodoro, mashuka, vyandarua pamoja na unga.

Kwa upande wake Mkuu wa Wilaya ya Tanganyika, Onesmo Buswelu amewaasa wananchi hao kutumia vizuri vyandarua vya kujikinga dhidi ya mbu waenezao ugonjwa wa malaria walivyopatiwa huku akiwapa onyo ya kutovulia samaki pamoja na kufugia kuku na endapo watabainika watachukuliwa hatua za kinidhamu.

Naye Mkuu wa Mkoa wa Katavi, Mwanamvua Mrindoko amesema kama mkoa wamekusanya mahitaji mbalimbali kutoka serikalini na kwa wadau mbalimbali wa maendeleo ili kugusa mahitaji ya wahanga wa mafuriko.

Amesema mahitaji hayo ni pamoja na vyakula vyenye thamani ya shilingi 113,278,271 ambavyo vimegawiwa kwa wahanga 4166 waliopatwa na madhara mkoani humo.

Nao baadhi ya Wananchi wa Halmashauri ya Wilaya ya Tanganyika walioathirika na mafuriko hayo wameishukuru serikali kwa misaada hiyo huku wakiiomba kuboreshewa baadhi ya miundombinu ikiwemo ya barabara na mitaro kwa ajili ya kupunguza tatizo hilo endapo litatokea kwa siku zijazo.

Habari kuu kwenye Magazeti ya leo Mei 3, 2024
Serikali yajipanga kuimarisha uzalishaji mbegu bora