Bodi ya Wakurugenzi ya Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Simba SC imekubaliana kutomfuta kazi kocha anayekinoa kikosi cha klabu hiyo kwa sasa, Pablo Franco Martin licha ya kutofikia malengo.
Pablo ambaye alijiriwa klabuni hapo akichukua nafasi ya Didier Gomez mwishoni mwa mwaka 2021, alisaini mkataba wa kufanya kazi Simba SC huku akipewa mtihani wa kuivusha Simba SC hatua ya Robo Fainali na kuipeleka Nusu Fainali Kombe la Shirikisho.
Baada ya mchezo dhidi ya Orlando Pirates Jumapili (April 24), tetesi za kuondoka kwa Kocha huyo kutoka nchini Hispania zilichukua nafasi kubwa katika mitandao ya kijamii, kwa kutumia kigezo cha kushindwa kufikia malengo aliyowekewa na viongozi wa Simba SC.
Simba SC ilitupwa nje ya michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa changamoto ya Mikwaju wa Penati 4-3, baada ya mchezo wao na Orlando Pirates kumalizika kwa matokeo ya jumla 1-1.
Katika hatua nyingine imeelezwa kuwa Kocha Pablo amepewa nafasi ya kupendekeza majina ya wachezaji ambao wataachwa mwishoni mwa msimu na wale atakaowahitaji kwa msimu ujao 2022/23.