Naibu Waziri wa Wizara ya Mambo ya ndani Jumanne Sagini amewataka Wamiliki na Watumiaji wa vyombo vya moto barabarani kuzingatia na kufuata sheria za usalama barabarani ikiwemo kulipa madeni wanayodaiwa bila kushurutishwa.

Ameyasema hayo leo April 27,2022 Jijini Dodoma wakati akizindua Mashine mpya za kisasa za (POS) kwa ajili ya kukusunyia Maduhuli ya jeshi la polisi hususani kitengo cha usalama barabarani pamoja na kutumika katika ununuzi wa silaha, Hati ya tabia njema na kukusanyia tozo mbalimbali barabarani hasa kwa madereva wasiofuata sheria za usalama barabarani.

Sagini ameongeza kuwa mashine hizo mpya zinatumia mfumo wa Android hivyo ina ‘Wireless’, inaskani leseni, ina uwezo wa kuchukua alama za vidole pamoja na kupiga picha jambo ambalo litasaidia kupunguza malalamiko ya wananchi yaliyokuwepo.

Mhe. Jumanne Sagini akizungumza na wadau wa usalama barabarani

Kutokana na hatua hiyo Sagini amewapongeza Jeshi la polisi nchini kwa kutumia wataalamu wake wa ndani kuendeleza mfumo huo ambao unakwenda kupunguzia jeshi hilo malalamiko na kuwafanya waweze kutekeleza majukumu yao bila kutumia nguvu kubwa kwa sababu mfumo huu kwa sasa unachukuwa taarifa za muhimu kwa Dereva hivyo hawezi kuja kukataa kwa sababu alama za vidole havifanani dunia nzima.

“Nawapongeza sana naamini mfumo huu utakwenda kuwa chanya kwenu na kwa wananchi hatutegemei kupata malalamiko tena ya kuwepo kwa makosa katika kumuandikia mtu kosa, amesema Mhe.Sagini.

Kwa upande wake Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Simon Sirro amewataka watumiaji wa barabara hususani madareva kutii sheria bila shuruti na kutoa ushirikiano pale Askari wa usalama barabarani wanapotaka kuchukua taarifa zao kwa ajili ya kujiridhisha wanapoandika ama kufanya ukaguzi wa vyombo vya moto.

“Kwa mashine hizi mpya inahitaji dereva achukuliwe alama za vidole,picha na kuskani leseni sasa niwaombe usiwe mbishi pale askari anapotaka taarifa hizi mtoe ushirikiano kikubwa tii sheria bila kushurutishwa,” amesema IGP Sirro.

IGP Sirro akizungumza na wadau wa usalama barabarani

Naye Mkuu wa kitengo cha TEHAMA (ICT) wa jeshi la polisi nchini ACP. Dawson Msongaleli amesema kuwa mfumo huo ulianza kwa kufanyiwa majaribio kwa mkoa wa Dar-es-salaam na Pwani mwaka 2017 baada ya kufanya kazi vizuri ndipo 2018 wakaanza kutumia kwa mikoa yote ya Tanzania Bara.

ACP Msongaleli amesema nia ya kutumia mashine hizi ni kuondokana na ule mfumo wa kujazana katika vituo vya polisi na kusababisha foleni isiyokuwa na maana na badala yake kila kitu kitafanyika kielektroniki

Kocha Pablo kuendelea Simba SC
Kanye West na Universal Music Kizimbani