Waziri wa Uwekezaji Viwanda na Biashara Dk. Ashatu Kijaji, amesema ni kosa la jinai kwa wafanyabiashara kupandisha bei za bidhaa na huduma kiholela, na kwamba itaanza kuwachukulia hatua za kisheria kwa mujibu wa kifungu cha 9 (1) cha Sheria ya Ushindani Na. 8 ya 2003.
Dk.Kijaji amesema amesema hayo wakati akiwasilisha makadiri ya Bajeti ya Wizara yake kwa Mwaka wa Fedha 2022/23, Bungeni Dodoma.
Ambapo amesema kuwa bei za vifaa vya ujenzi ikiwemo mabati na nondo zimeendelea kuwa juu sambamba na ongezeko la bei za mazao ya chakula nchini.
Dk. Kijaji amesema wastani wa bei ya maharage imepanda kutoka Sh 177,340 kwa gunia la kilo 100 mwezi Machi 2021, hadi Sh. 188,294 mwaka 2022. Wastani wa bei ya mahindi kwa gunia la kilo 100 imeongezeka kutoka Sh 48,341 hadi Sh 59,861.
Amesema wastani wa bei ya bati la geji 30 imepanda kufikia Sh.27,714 mwezi Machi 2022 kutoka Sh. 20,786 wakati nondo moja ya mm 12 imepanda kutoka Sh 20,393 hadi Sh. 26,875 katika kipindi cha matazamio.
“Mwenendo wa bei ya mafuta ya kula katika soko la dunia imeendelea kupanda kutokana na Janga la UVIKO-19 na athari ya vita ya Urusi na Ukraine,” Waziri Kijaji amesema.