Baada ya kutoka agizo la kufungiwa kwa video ya wimbo ‘Mtasubiri’ wa msanii Diamond Platnumz aliomshirikisha Zuchu, kutoka Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania, TCRA kwa kushirikiana na Baraza la Sanaa la Taifa, hatimaye wasanii hao wamejitokeza na kuonesha hisia zao.
Kupitia ukurasa wake wa Instagram Zuchu ameandika barua ya wazi yenye ujumbe mrefu kwa mamlaka hizo kwa kuambatanisha na baadhi ya video zilizowahi kufanywa na wasanii wa Tanzania zikiwa na maudhui sawa na hayo bila ya kupigwa marufu.
“Ni matumanini yangu mpaka sasa kila mtu anafahamu kua Video Ya wimbo wetu pendwa ‘MTASUBIRI’ Umesitishwa kuonekana kwenye vyombo vya habari Nchini kwetu. Nimeona bora nianze moja kwa moja kwenye mada husika .Jana Nilipokea taarifa hizi kupitia mitandao kama nyinyi tu mashabiki zetu kwamba wimbo wetu unapigwa marufuku sababu tajwa kua inaleta ukakasi kwenye jamii husika mwisho wa kununukuu.
Awali ya yote niseme kama msanii nilietumia ubunifu kukaa chini na muongozaji wa video yetu takribani siku 4 kuunda stori ambayo kwa utashi wangu na heshima niliyonayo kwa dini zote na madhehebu yake sikuona huu ukakasi unaoongelewa hapa, Nafahamu si kila kazi ya kisanaa itamfurahisha kila mtu lakini kuvunjia heshima dini si kitu ambacho kipo ndani ya weledi wa kazi yetu sababu tunafahamu fika tunao mashabiki wa dini zote na kulinda hisia zao ni moja ya nguzo kuu Kwenye mziki hatueki matabaka.
Ifahamike kwamba mimi ndie nilishoot hiyo scene ikinitaka kuwepo kanisani nikiwa nafanya mazoezi ya kwaya sio misa ni mazoezi ya kikwaya nikiwa nimevalia joho lenye stara. Kanisa hili lipo kisarawe na kabla ya kushoot masister walitukagua na kusikiliza kwa makini stori yetu na kuridhishwa nayo ndipo hapo tukapewa ruhusa ya kushoot. Naomba nielekeze malalamiko yangu kwa mamlaka husika BASATA walezi na wazazi nimeambatanisha video na movie baadhi ambazo zimetoka kabla ya mtasubiri vipi hizi hazina ukakasi.
Lakini ni jamii ipi hiyo iliyoleta malalamiko mpaka nyie kufungia video iliyogharimu muda wa siku nne na pesa nyingi kuishoot tena mkaifungia bila hata kutaka kusikiliza utetezi, Mtasubiri video ni ya kawaida sana A very innocent sweet story, Naumia sababu hii inaenda kudumaza sio tu mziki ila Tasnia nzima kwa ujumla. HAYATI baba wa taifa alisema ‘Utii ukizidi huzaa uoga ,Uoga huzaa unafiki na kujipendekeza mwisho wake Umauti’. Huu ndio umauti wa Tasnia hii unapoanzia” ameandika Zuchu
Muda mfupi baada ya ujumbe huo mrefu, mwanamuziki Diamond naye kupitia sehemu ya comment kwenye chapisho la Zuchu aliweka ujumbe wa kuunga mkono alichozungumza Zuchu huku akiwasilisha mtazamo wake na nama alivyopokea taarifa za kufungiwa kwa video hiyo.
“Najiuliza kuna baya lolote limefanyika kwenye hio scene? Mlivaa vimini? hapana!… Nlitwerk ama Mliimba matusi humo kanisani? Hapana!.. Mlivuta sigara au bangi humo? Hapana!… Mlikiss ama Kunywa Pombe humo Hapana, Simu iliita, ulipokelea ndani? Hapana…je kushoot kanisani ni sisi wa kwanza? hapana! Kuna wengine walishoot Videos na Movie tena wao walifanya kwa kulidhalilisha kabisa kanisa… Nyimbo zao Zili fungiwa??? hapana!, Halafu kesho utaniuliza kwanini Nilikataa kushiriki Tuzo za Basata” Ameandika Diamond.
Video ya wimbo huo yenye jumla ya watazamaji zaidi ya Milioni 10 kwenye mtandao wa YouTube, uliachiwa rasmi Machi 29, 2022, ikiwa ni moja ya nyimbo kutoka kwenye Extended playlist ‘EP’ mpya ya nyota huyo iitwayo ‘First of all’.