Siku moja baada ya kuanza Kambi mkoani Shinyanga kwa ajili ya maandalizi ya Nusu Fainali Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ dhidi ya Mabingwa Watetezi Simba SC, Kocha Mkuu wa Young Africans Nasreddine Nabi amewatimua Saido Ntibazonkiza na Dickson Ambundo.
Kwa mujibu wa taarifa iliyoandikwa kwenye tovuti ya Mwanaspoti imeeleza kuwa, sababu za kutimuliwa kwa wachezaji haio ni kutoroka kambini na kwenda mtaani kinyume na utaratibu.
Hadi sasa Uongozi wa Young Africans haujasema lolote kuhusu tukio hilo, ambalo limekua likipigwa vita kwa lengo la kulinda msingi wa nidhamu kwenye kikosi cha klabu hiyo inayokaribia ubingwa wa Tanzania Bara.
Simba SC na Young Africans zitakwaana Jumamosi (Mei 28), katika Uwanja wa CCM Kirumba jijini Mwanza zikiwa na kumbukumbu ya kugawana alama kwenye michezo miwili ya Ligi Kuu msimu huu 2021/22.
Simba SC imeweka Kambi wilayani Misungwi, na inafanya mazoezi yake katika Uwanja wa Gwambina Complex unaomilikiwa na klabu ya Gwambina inayoshiriki Ligi Daraja la Kwanza Tanzania Bara.
Simba SC ilitinga Nusu Fainali ya ASFC kwa kuichapa Pamba FC mabao 4-0, huku Young Africans ikiitoa Geita Gold FC kwa changamoto ya Penati baada ya kutoshana nguvu ndani ya dakika 90.