Msafara wa wachezaji 23 wa Azam FC umeondoka Jijini Dar es salaam kwenda Arusha tayari kwa mchezo wa Nusu Fainali ya Pili Kombe la Shirikisho Tanzania Bara ‘ASFC’ utakayopigwa Jumapili (Mei 29) Uwanja Sheikh Amri Abeid dhidi ya Coastal Union.

Nusu Fainali ya Kwanza ya ‘ASFC’ itachezwa Jumamosi jijini Mwanza katika Uwanja wa CCM Kirumba, kati ya Bingwa mtetezi Simba SC dhidi ya mtani wake Young Africans.

Azam FC iliyotinga hatua ya Nusu Fainali ‘ASFC kwa kuichapa Polisi Tanzania, imeondoka na matumaini makubwa ya kwenda kupambana na kupata ushindi utakaowavusha hadi hatua ya Fainali, itakayopigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid mapema mwezi Julai.

Kocha wa Mkuu wa Azam FC, Abdihamid Moallin amesema wanakwenda Arusha kupambana, huku wakifahamu mchezo utakua mgumu kutokana na uhodari wa wapinzani wao kutoka jijini Tanga.

Amesema amekiandaa vyema kikosi chake kwa ajili ya kupambana ndani ya dakika 90, huku lengo lao kubwa likiwa ni kusaka ushindi utakaowavusha hadi Fainali ya ‘ASFC’.

“Tunaondoka tukiwa na matumaini makubwa ya kupambana na kupata ushidni katika mchezo wetu wa Jumapili, tunaijua Coastal Union, ina kikosi Bora na Imara, hivyo tumejiandaa kwa kila hali ili kupambana nayo.”

Katika hatua nyingine Kocha huyo kutoka Marekani mwenye asili ya Somalia amethibitisha kuachwa kiungo Ibrahim Ajibu jijini Dar es salaam, sanjari na wachezaji wengine tisa.

“Wachezaji waliobaki ni pamoja na Ibrahim Ajib, Mathias Kigonya, Nicholaus Wadada, Abdul Haji Omar, Khlefin Hamdoun,, Yahya Zayd, Frank Domayo na Emmanuel Kaberege wameachwa kutokana na sababu za kiufundi”

Moallin amesema wengine ambao wameshindwa kusafiri na timu ni: Prince Dube, Ayoub Lyanga na Idd Seleman ‘Nado’ ambao wote wanasumbuliwa na majeraha.

Mwenyekiti Simba SC amshangaa Bernard Morrison
Habari kuu kwenye magazeti ya leo Mei 27, 2022