Idadi ya watu waliofariki kwenye ajali ya Basi dogo lililogonga Lori lililokuwa limeharibika barabarani eneo la Mafinga Wilayani Mufindi Mkoani Iringa, imefikia 20.
Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Iringa, ACP Allan Bukumbi amesema chanzo cha ajali hiyo iliyotokea leo Juni 10, 2022 ni uzembe wa dereva wa basi dogo lililokuwa linatoka Mkoani Dar es Salaam kwenda Mbeya.
Kamanda Bukumbi amesema, Dereva wa Basi dogo alipoteza mwelekeo na kushindwa kulimudu gari na kisha kuligonga roli ambalo lilikuwa limeegesha baada ya kupata ajali kwenye eneo hilo jirani na Changarawe.
“Abiria walionusurika wakati wakiwaokoa majeruhi, lori jingine likaja na kuwagonga abiria waliokuwa wakiokolewa kwenye ajali ya kwanza na kusababisha vifo vingi zaidi” amesema Kamanda Bukumbi.
Mkuu wa Wilaya ya Mufindi, Saad Mtambule amesema hali za majeruhi zinaendelea vizuri na kuongeza kuwa wengine wamehamishiwa katika hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa kwa matibabu zaidi.
Amesema, kutokana na ufinyu wa chumba cha kuhifadhia maiti katika Hospitali ya Mafinga, wamelazimika kuhamisha miili 12 ya waliofariki na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti cha Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Iringa.
“Tumelazimika kufanya hivi kutokana na ufinyu wa chumba cha maiti na sasa ndugu watalazimika kwenda Hospitali ya Mkoa Iringa ili kuwatambua miili ya marehemu.
Mapema hii leo Juni 10, 2022 Rais Samia Suluhu Hassan, ametuma salamu za rambirambi kwa Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Queen Sendinga kutokana vifo vilivyotokana na ajali hiyo.
Taarifa iliyotolewa na Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais Ikulu, ZuhuraYunus imesema Rais Samia pia anawapa pole wafiwa na anaungana na familia zao katika kipindi hiki cha majonzi.