Mzee mmoja Joseph Gendamwene (80), ameituhumu Serikali kumcheleweshea kifo chake kwa kushindwa kutatua mgogoro wa ardhi uliopo baina ya Shirika la Watawa la Imiliwaha na wakazi wa kijiji cha Madobole kilichopo Wilaya na Mkoa wa Njombe.

Mzee Gendamwene ameyasema hayo katika mkutano wa hadhara ulioitishwa na Mkuu wa Wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa katika ziara yake ya kusikiliza kero mbalimbali za Wananchi na kuzitafutia ufumbuzi.

“Mkuu wa wilaya nitakusifu sana endapo utayafanyia kazi maagizo yangu maana unanichelewesha kufa mimi nimeahidiwa kufa endapo mgogoro huu wa eneo utaisha,” alisema Mzee huyo.

Bila kuwataja watu waliompa ahadi ya kifo, Mzee huyo amesisitiza umuhimu wa Serikali wa kutatua migogoro ya wananchi ikiwemo wa Kijijini kwake Madobole dhidi ya watawa, wakigombea mpaka wa shamba lenye ukubwa wa ekari 1026.

Akijibu hoja hiyo, Mkuu wa wilaya ya Njombe, Kissa Kasongwa amewataka wananchi wa eneo hilo kuendelea kuwa wavumilivu kwani Serikali ipo katika harakati za utatuzi wa jambo hilo.

Hata hivyo, Mkuu huyo wa Wilaya alifika eneo la tukio akiwa na wahusika wa pande zote mbili za mgogoro huo, na kusema historia inahukumu kwa kuwa Wazee hao wakongwe wanaeleza jinsi Watawa hao walivyowakuta na kuwapokea.

“Ni lazima tuangalie hili jambo maana wazee wetu wanasema mlifika wakawapokea na wakawapa eneo lakini baadae kwa utaratibu wa kiserikali mkaongeza ukubwa sasa wao hawafahamu hivyo inabidi tutumie busara katika hili,” alisema Mkuu huyo wa Wilaya.

Akiongea kwa niaba ya watawa Sista mmoja ambaye hakutaja jina lake, amesema inabidi yafanyike maombi ya kimaandishi ili waweze kukaa na kujadiliana na kupata muafaka.

Mbali na kuongea na wananchi kusikiliza kero zao na kuzifanyia kazi, Mkuu huyo wa Wilaya pia anaendelea na ziara ya ukaguzi wa miradi ya maendeleo katika maeneo mbalimbali ya Halmashauri ya Wilaya ya Njombe.

Sakata la figo, familia yaikataa ripoti ya ikulu
Kombe la Ubingwa Ligi Kuu 2021/22 laanikwa hadharani