Umoja wa Mataifa ya Ulaya (EU), umesisisitiza udumishwaji wa suala la Demokrasia, Amani na uwepo wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa ya Zanzibar, kwa lengo la kujenga na kuendeleza ushirikianao na mahusiano yaliyopo.
Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman ameyasema hayo baada ya kikao chake na Ujumbe wa Umoja huo wa Ulaya uliofika ofisini kwake Mjini Zanzibar, kujitambulisha na kufanya mazungumzo.
“Wametaka kujua namna ambavyo tunashughulikia maridhiano ya umoja wa Kitaifa na uundwaji wa vyombo vyake vya usimamizi na matarajio yalivyo katika mahusiano baina yetu na umoja huu,” amesema Makamu wa Kwanza wa Rais.
Katika kutekeleza mpango rasmi wa Umoja wa kitaifa na maridhiano Zanzibar, Makamu wa kwanza Rais akaelezea maeneo kadhaa yanayohitajika kufanyiwa kazi na Umoja huo, ikiwemo suala la ushughulikiaji wa vyombo vya usimamizi wa maridhiano.
“Mojawapo ni kufanya mageuzi katika taasisi zinazoshughulikia umoja huu ikiwemo Mahakama na vyombo vingine vya sheria na eneo jingine ni la suala la mageuzi katika Serikali za mitaa ili wananchi washiriki vyema shughuli za ujenzi wa nchi yao,” amefafanua Makamu wa Rais Othman.
Kwa upande wake Mwakilishi Kiongozi wa Baraza la Ulaya Barani Afrika, Bi. Yemina Gierfi, amesema moja ya malengo makuu ya ujumbe wao ni kukutana na Viongozi mbalimbali, ili kujifunza na kuimarisha ushirikiano baina ya Mataifa na Umoja huo wa Ulaya.