Askofu Mkuu wa Kanisa Katoliki Jimbo kuu la Mbeya, Gervas Nyaisonga amethibitisha kupatikana kwa mwili wa Padre wa Wamishionari wa Afrika (White Father), Michael Samson uliookotwa eneo la sabasaba karibu na mto Meta jijini humo.

Taarifa ya Rais wa Baraza la Maaskofu Tanzania (TEC), Gervas Nyaisonga imesema Padre Samson alitoweka Ijumaa Juni 10 mwaka huu katika kituo cha Vijana cha Kanisa Katoliki Mbeya saa 12.30 jioni, na mwili wake kupatikana Juni 11, 2022.

“Padre Michael alitoweka Juni 10, 2022 majira ya saa 12.30 jioni na mwili wake kupatikana Juni 11, 2022 majira ya saa 4:00 asubuhi maeneo ya Sabasaba jijini Mbeya” ilisema taarifa hiyo.

Bado Jeshi la Polisi halijathibitisha kutokea kwa tukio hilo na mazingira ya kifo husika, ingawa baadhi ya ya mashuhuda wamedai mwili wa Padre huyo ulikuwa umefungwa kwenye blanketi wakati ukiokotwa.

Wakati huo huo, Kamanda wa Polisi kanda maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema wanamsaka raia wa China Zheng Lingyao (42), mkazi wa Dar es salaam anayetuhumiwa kumuua raia mwenzake Fu Nannan, (26).

Muliro amesema tukio hilo limetokea Juni 11 majira ya saa 5:45 usiku katika mtaa wa Kalenga, Ilala jijini Dar es salaam, eneo alilokuwa akiishi marehemu.

“Mtuhumiwa alifika eneo hilo na kumjeruhi kwa risasi tumboni mwanamke mmoja Nie Mnqin naye ni raia wa China na baada ya kumjeruhi mwanamke huyo alimfyatulia risasi Fu Nannan,” alisema Muliro

Mwanamke huyo majeruhi Mnqin, anaendelea na matibabu katika hospitali ya Taifa Muhimbili na uchunguzi wa awali umebaini tukio hilo linahusisha mambo ya kimapenzi.

Habari kuu kwenye magazeti ya leo Juni 13, 2022
Wamiliki magari ya abiria watakiwa kuwa na leseni za usafirishaji