Mkuu wa Mkoa Arusha, John Mongella amethibitisha kifo cha askari mmoja ambaye alifariki jana Juni 10, 2022, kwa kupigwa mshale na kundi la watu wenye silaha wakati wa zoezi la uwekaji wa alama za mipaka, katika eneo la Loliondo lililopo Wilayani Ngorongoro.

Mongella ameyasema hayo hii leo Juni 11, 2022 wakati akizungumzia kile kinachoendelea katika eneo la hilo la Loliondo na kuonya juu ya taarifa zenye lengo la kuchochea vitendo viovu.

“Tupo loliondo hapa hali ni shwari tunaweka alama za mipaka katika eneo la kilometa 1,500 kwa ajili ya eneo nyeti la mazalia, kulinda chanzo cha maji na mapito ya wanyama, kwa bahati mbaya tu alasiri ya jana askari mmoja aliuawa kwa kupigwa mshale,” amesema Mongella.

Amesema, kundi la watu ambalo lilitaka kuathiri utekelezaji wa zoezi hilo lilifika mahala hapo na kumpiga mshale Askari huyo mzalendo, ambaye wanathamini na kutambua mchango wake wa kutetea maslahi ya Taifa akiwa kazini.

“Pamoja na kauli nzuri ya Waziri Mkuu Bungeni jana asubuhi (Juni 10, 2022), alasiri tukapata tukio hilo lakini kwasasa zoezi linaendelea vizuri na baada ya kuweka alama, maeneo hayo yatakuwa shirikishi kwa wananchi,” amesisitiza Mongella.

Aidha, amesisitiza kuwa mpaka sasa kwenye maeneo ya hospitali na vituo vya afya hakuna majeruhi, ingawa kwenye mitandao wapo watu wanaochapisha picha za miaka mingi na baadhi zimetambuliwa kuwa ni za miaka mitatu iliyopita.

“Serikali yetu ni ya utawala wa sheria kama kuna mtu ana majeraha ajitokeze atibiwe lakini tungependa suala la upotoshaji lisiendelee, tunafanya jambo la kimaendeleo kwa mustakabali wa wananchi, jamii na maslahi mapana ya nchi,” amesema Mkuu huyo wa Mkoa.

Juni 10, 2022 Bungeni jijini Dodoma, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa alisema kumekuwa na upotoshaji kuhusu kinachoendelea Tarafa ya Loliondo na kukemea tabia hiyo huku akitaka vyombo vya dola kuwasaka watu hao.

Tangu Juni 9-10, 2022, kumekuwa na picha mnato na za video zinazosambaa kwenye mitandao ya kijamii, zikionyesha Wamasai wenye silaha za jadi ikiwemo mapanga na mishale zinazoelezewa kuwa wamejiandaa kukabiliana na yeyote mwenye kutaka kugusa ardhi yao.

Shambulizi la anga laua zaidi ya 50 Nigeria
OACPS yatangaza neema kwa wakulima