Mwandishi wa Kitabu cha “How to Murder Your Husband,” Nancy Crampton-Brophy (71), amehukumiwa kifungo cha maisha jela kwa kupatikana na hatia ya mauaji ya mumewe.
Crampton-Brophy amehukumiwa kifungo hicho Juni 13, 2022 na alishtakiwa mwezi Mei 2022, kwa mauaji ya mumewe, Daniel Brophy (63), mpishi ambaye aliuawa kwa kupigwa risasi akiwa katika taasisi ya Culinary Oregon Juni 2018.
Katika stakabadhi za Mahakama, waendesha mashtaka wamesema Daniel Brophy, alipigwa risasi mbili, moja eneo la mgongoni wakati amesimama kwenye sinki la kujaza barafu na ndoo za maji kwa ajili ya wanafunzi, na nyingine kifuani.
Waendesha mastaka hao wamesema Crampton-Brophy alimuua mumewe ili apate bima ya zaidi ya dola milioni moja na walihoji juu Mwandishi huyo kuwa na nia ya kumuua mumewe kutokana na changamoto za kifedha, na kupokea malipo makubwa ya bima baada ya kifo chake.
Mbele ya Mahakama, waendesha mashtaka hao waliambia Mahakama kuwa mwandishi huyo alimfuata mumewe kazini na kumpiga risasi na bunduki aina ya Glock, ambapo Crampton Brophy alionekana akiendesha gari akiingia na kutoka kazini kwa mume wake wakati wa uhalifu huo katika picha za CCTV zilizoonyeshwa mahakamani.
Inadaiwa kuwa Wapelelezi walipata maganda mawili ya risasi kwenye eneo la tukio, na kwamba mtuhumiwa alikuwa amenunua kifaa cha kuunganisha cha “ghost gun” (bunduki ambazo hazijasajiliwa na haziwezi kunaswa), AMBACHO wachunguzi waliKIpata baadaye.
Akijitetea mbele ya Mahakama, Crampton-Brophy alisema alinunua bunduki aina ya ghost-gun kama sehemu ya utafiti wa kitabu kipya na si kwa ajili ya kumuua mumewe.
Habari za mauaji hayo na mashtaka ya jinai dhidi yake zilienea kila mahali kwa kasi kutokana na insha aliyoandika Crampton-Brophy miaka saba kabla ya kifo cha mumewe.
Mwaka 2011, aliichapisha insha maarufu katika blogi iitwayo See Jane Publish, iliyogawanywa katika sehemu zinazoelezea faida na hasara za kumuua mume mwovu.
Jaji aliyesikiliza kesi hiyo alisema kuwa insha hiyo haitaruhusiwa kuwa ushahidi kwa sababu iliandikwa miaka mingi iliyopita kama sehemu ya semina ya uandishi na inaweza kuathiri visivyo haki baraza la mahakama.