Mapendekezo ya kufutwa kwa ada ya wanafunzi wa kidato cha tano na sita yaliyotolewa na Serikali na kuwasilishwa Bungeni na Waziri wa Fedha Dk Mwigulu Nchemba yamewaibua baadhi ya Wazazi, wananchi na wadau ambao wamesifu mpango huo.

Kupitia mahojiano na baadhi ya makundi hayo ya kijamii, wamesema baada ya Waziri Nchemba kusoma mependekezo ya Bajeti ya Serikali ya Mwaka 2022-2023 ambayo pamoja mambo mengine imependekeza kufutwa kwa ada hiyo ni wazi itasaidia kupunguza mzigo wa ada kwao.

“Huu ni muendelezo wa nafuu anayotupatia Rais Samia Suluhu Hassan tangu aapishwe kwa mujibu wa katiba kuwa Rais wetu inatia faraja sana maana kama unafanyia jambo linalokupa ahueni kushukuru ni ibada,” alisema mzazi Zawadi Mbega mkazi wa Tabata Kifuru.

Amesema binafsi kama mzazi hana cha kusema zaidi ya kuiombea heri Serikali katika kutimiza majukumu yake ya kuwatumikia Watanzania, na kwamba kinachofuata ni kuwasisitiza watoto kuzingatia masomo kwani si vyema kuchezea pesa ya kodi za Watanzania.

Kwa upande wake Bi. Mwajuma Ubwa mkazi wa Tubuyu Mkoani Morogoro amesema wanaishukuru Serikali kwa hatua hiyo ambayo inaenda kuyafuta machozi ya watazania wengi wenye vipato vya chini na kusema Wazazi sasa wanapaswa kuwa karibu na watoto ili waweze kuwahimiza kupenda shule.

“Bure ina gharama yake nina uhakika kabisa wapo wazazi ambao wataachana na habari za kufuatilia maendeleo ya watoto maana si elimu bure, tumezoe tukilipa na maneno juu kwa watoto sasa hofu yangu tutaiachia kila kitu Serikali we utanijionea,” alisema Mama huyo kwa msisitizo.

Awali akichangia mjadala huo, Mzee Masoud Tengelakwi wa Biafra Kinondoni jijini Dar es salaam amesema huu ni mwendelezo wa kile alichokifanya aliyekuwa Rais wa awamu ya Tano Hayati Dkt. John Magufuli, baada ya kufuta ada kwa wanafunzi kuanzia kidato cha kwanza hadi cha nne hivyo Rais Samia anapaswa kupongezwa kwa kumalizia kazi.

“Kuna mema yakianzishwa huwa yanatupiliwa mbali au mtu akiyafuata anaonekana ameiga hivyo wengine huachana na hiyo dhana lakini kwa Rais samia jambo hili kwake ni msamiati ye akiona jema anahangaika nalo mpaka aone matokeo na huu ndio uongozi,” alifafanua Tengelakwi.

Akisoma mapendekezo ya bajeti ya Serikali ya Mwaka 2022-2023 Juni 14, 2022 Bungeni jijini Dodoma, Waziri wa Fedha Dkt. Mwigulu Nchemba alisema katika utekelezaji wa bajeti hiyo, Rais Samia alitoa mapendekezo ya kuondolewa kwa ada hiyo.

Augustine Okrah anukia Msimbazi
Mwandishi "how to murder your husband" jela maisha