Mtu mmoja Edward Motaroki Nyaanga anayedaiwa kujifanya afisa wa Polisi wa Makao Makuu ya Jeshi la Polisi nchini Kenya amefikishwa Mahakamani kwa makosa ya kumpiga na kumjeruhi afisa halisi wa Polisi na kujifanya afisa wa jeshi hilo.
Kwa mujibu wa hati ya mashtaka, Nyaanga alifanya tukio hilo Juni 16, 2022 katika mtaa duni wa Southlands mtaani Lang’ata kaunti ya Nairobi, kwa kumpiga Konstebo Dominic Obura wakati akiwa doria na kumsababishia majeraha kichwani na mikononi kwa kujifanya afisa wa Polisi.
Upande wa mashtaka umesema, mtuhumiwa ambaye alionekana kuwa mgeni alimwita konstebo Obura na kumwambia alikuwa afisa wa polisi kutoka makao makuu ya polisi na kutakiwa kujitambulisha kwa kutoa kitambulisho cha kazi, lakini badala yake akaanza kumshambulia.
Hata hivyo, inadaiwa badaye Afisa huyo wa polisi aliokolewa na wenzake ambao walimkamata mtuhumiwa Nyaanga na kumfikisha katika kituo cha polisi cha Lang’ata.
Mbele ya Hakimu Mkuu wa Kibera, Ann Mwangi mshtakiwa alikana mashitaka hayo na kupitia kwa wakili wake Mwihaki Ng’ang’a, Nyaanga aliomba mahakama kumhurumia na kwamba mtuhumiwa huyo hana rekodi ya makosa, ni baba wa familia na mwananchi mtiifu.
Mtuhumiwa huyo yupo nje kwa dhamana ya pesa taslimu Shilingi 30,000 na kesi yake itatajwa tena Juni 28, 2022.