Halmashauri ya jiji la Dar es salaam inatarajia kupokea wageni zaidi ya 30 kutoka jiji la Hamburg nchini Ujerumani ikiwa ni ziara ya kuadhimisha miaka 12 ya mahusiano ya majiji hayo mawili.
Kwa mujibu wa Mkurugenzi wa jiji, Halmashauri ya jiji la Dar es salaam, Jumanne Shauri amesema wageni hao wanatarajia kuwasili Juni 30, 2022 na maadhimisho hayo yanatarajia kuanza siku ya kuwasili hadi kilele chake Julai 3, 2022.
“Siku ya Alhamisi tarehe 30 juni, 2022 jiji la Dar es salaam linatarajia kupokea ujumbe wa wageni zaidi ya 30 kutoka jiji la Hamburg nchini Ujerumani wanaokuja kwenye ziara ya kuadhimisha miaka 12 ya uhusiano wa majiji haya,” amesema Shauri.
Amesema, uhusiano wa miji dada kati ya jiji la Dar es salaam na jiji la Hamburg ulianza Julai 1, 2010 baada ya mamlaka zote mbili kuridhia kuanzishwa kwa uhusiano huo na kwamba ugeni huo ni muhimu katika kusherehekea mafanikio ya utekelezaji wa miradi mbalimbali.
Mkurugenzi Shauri ameyataja mafaniko hayo yaliyofikiwa kwa pamoja kuwa ni utekelezaji wa miradi ya Mabadiliko ya tabia nchi, Afya, Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Utamaduni wa Michezo, Utalii na Elimu.
“Mafanikio mengine ni pamoja na Stadi za kazi za Wanawake, Vijana na watu wenye mahitaji maalum, na ugeni huu ni muhimu katika maadhiisho haya ambayo kilele chake ni Julai 3, 2022,” amesema Mkurugenzi huyo.
Kwa mujibu wa ratiba ya maadhimisho hayo, siku ya ijumaa Julai 1, 2022 viongozi wa majiji hayo mawili watasaini makubaliano ya kudumisha uhusiano wao kwa kutoa nafasi kwa wadau wengi kunufaika na fursa zitakazojitokeza.
Awali maadhimisho haya yalipangwa kufanyika mwaka 2020, lakini ilishindikana kutokana na janga la UVIKO-19, huku wananchi wakikaribishwa katika viwanja vya Mnazi mmoja kushiriki na kutumia fursa hiyo kwa manufaa ya jiji.