Klabu ya Azam FC inatajwa kuwa kwenye mpango wa kuacha theluthi ya wachezaji wake, kuelekea msimu mpya wa Ligi Kuu na Michuano ya Kimataifa (Kombe La Shirikisho Afrika).
Klabu hiyo yenye Maskani yake Chamazi jijini Dar es salaam, inajipanga kufanya maamuzi hayo, kufuatia kushindwa kufikia malengo iliyokuwa imejiwekea msimu wa 2022/23, ambao unakwenda ukingoni.
Hata hivyo wachezaji Edward Manyama aliyesajiliwa kutoka Ruvu Shooting na Yahya Zayid aliyekua anacheza soka nchini Misri, wanatajwa huenda wakatolewa kwa mkopo, huku wengine tisa wakitarajia kuondoka jumla.
Wanaotajwa huenda wakaondoka jumla wazawa ni Frank Domayo aliyemaliza mkataba wake na Ibrahim Ajibu aliyesajiliwa wakati wa Dirisha Dogo akitokea Simba SC.
Wengine wanaotoka nje ya nchi ambao ni Mathias Kigonya, Nico Wadada, Paul Katema, Indriss Mbombo na Charles Zulu.
Kuondoka kwa wachezaji hao kutatoa nafasi kwa Azam FC kufanya usajili wa wachezaji wapya, ambao watakuwa na jukumu zito la kuipa heshima klabu hiyo kwa kupambana hadi kutwaa mataji msimu ujao wa 2022/23.