Serikali, imezindua Mradi wa uandaaji wa lishe bora ya gharama nafuu itakayonenepesha Ng’ombe nchini, uliofanyika kwenye ofisi za Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI), kanda ya Mashariki.

Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Tixon Nzunda amesema mradi huo unalenga kuongeza uzalishaji wa nyama bora, ambazo zitakuwa malighafi kwenye viwanda, lishe bora kwa wananchi na kupunguza pengo la vyakula vya mifugo.

Amesema upunguzaji wa pengo la vyakula vya mifugo utatokana na utengenezaji wa mashamba makubwa ya utafiti na mashamba darasa ya malisho, ili wafugaji waweze kupata elimu ya usindikaji wa mazao ya Mifugo.

“Nimeona kazi nzuri mnazozifanya hasa kwenye kituo cha unenepeshaji wa Mifugo ya Nyama, ule ni mfano mzuri wa kuigwa, tunataka vituo hivyo viwe vingi zaidi, tuwawezeshe vijana wanaotoka vyuoni,” amesema Nzunda.

Amesema, tayari wameandaa mpango wa mabadiliko ya Sekta ya Mifugo, ili kuimarisha huduma za afya ya Mifugo, kupata masoko ya uhakika ya Mifugo na bidhaa za Mifugo.

“Pia kutakuwa na mfumo imara wa upatikanaji wa masoko na mfumo imara wa upatikanaji wa malisho kwa kuwaruhusu sekta binafsi kushiriki mafunzo haya ili kusaidia kusonga mbele na kufikia lengo,” amesisitiza Katibu.

Awali Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Utafiti ya Mifugo (TALIRI), Prof. Erick Komba amesema taasisi hiyo ilianzishwa kwa lengo la kusimamia na kufanya tafiti za Mifugo, kuibua, kutathimini na kusambaza teknolojia bora.

“Tunafanya tafiti za malisho, tafiti za vyakula za Mifugo, uzazi wa Mifugo, uzalishaji wa Mifugo na tafiti za mbali za mbegu za Mifugo zinazowezeshwa na Serikali Kuu, wadau wa maendeleo kutoka ndani na nje ya nchi,” amefafanua Prof. Komba.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Taasisi ya Utafiti wa Mifugo (TALIRI), Kanda ya Mashariki, Tanga, Dkt. Zabron Nziku amesema mradi huo una thamani ya shilingi milioni 120 na msingi wake ni kutengeneza lishe bora ambayo itaweza kusaidia upatikanaji wa nyama bora.

Uzinduzi wa mradi wa uandaaji wa lishe bora ya gharama nafuu kwa unenepeshaji wa Ng’ombe Tanzania ulishirikisha wadau mbalimbali wakiwemo Viongozi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi (Mifugo), Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Tanga, Maafisa mifugo kutoka Halmashauri za Mkoa wa Tanga, watengenezaji wa vyakula vya Mifugo, Wanenepeshaji, wafugaji pamoja na wafadhili wa Mradi.

Habari kuu kwenye magazeti ya leo June 25, 2022
Panga kali kupita Azam FC, Ajib ndani