Waziri wa Uwekezaji, Viwanda na Biashara, Dkt. Ashatu Kijaji amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Cuba, Bruno Rodriguez Parrilla na kujadiliana juu ya uwezekano wa ukuzaji wa kiwanda cha kuzalisha viwatilifu ili kupata mbolea na bidhaa nyingine.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam hii leo Juni 30, 2022, Waziri Kijaji amesema moja ya bidhaa ambayo itazalishwa kiwanda hicho kilichopo Kibaha mkoani Pwani ni mbolea ambayo itatosheleza mahitaji kwa Taifa.
“Kilimo kinachangia kwa kiwango kikubwa kwenye uchumi wa Taifa letu hivyo mbolea ni moja ya ya malighafi muhimu kuhakikisha kilimo kinakuwa na mchango mkubwa nchini na sisi kama Wizara tuko tayari kuhakikisha kiwanda chetu kinaendelea na uzalishaji wa bidhaa hizi muhimu kwaajili ya maendeleo,” amesema.
Hata hivyo, Dkt. Kijai amesema kilichotakiwa ni kufanya majadiliano kati ya Serikali ya Tanzania na Cuba, na kwamba waliunda timu kwa nchi zote mbili ili kukaa meza moja na timu ya wataalamu kwa matarajio ya ufanikishaji wa lengo lilikosudiwa.
Awali, Balozi wa Tanzania nchini Cuba, Valentino Mlowola amesema ugeni huo utasaidia kukuza ushirikiano na kufanikisha upanuzi wa kiwanda hicho kitakachosaidia upatikanaji wa ajira kwa wananchi walio wengi ikiwemo kukuza sekta ya biashara nchini.
“Uhusiano wetu na Cuba ni mzuri na unaendelea kuimarika siku hadi siku na wataendelea kushirikiana kwenye sekta mbalimbali hususani kwenye sekta ya afya, Elimu pamoja na Viwanda,” amebainisha Balozi Mlowola.