Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Prof. Adolf Mkenda na Waziri wa Elimu wa Afrika Kusini, Matsie Angeline Motshekga wamesaini Hati ya Makubaliano ya Kufundisha Kiswahili katika Shule za Awali za Afrika Kusini.
Tukio hilo, limeongozwa na mgeni rasmi Makamu wa Rais wa Tanzania, Dkt. Philip Isdor Mpango katika Madhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani, yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mwalimu Julius Nyerere jijini Dar es Salaam, hii leo Julai 07, 2022.
Maadhimisho haya, yanafanyika kwa mara ya kwanza nchini kufuatia Shirika la Umoja wa Mataifa la elimu, sayansi na utamaduni (UNESCO), kuridhia kiswahili kuwa lugha rasmi kutumika Kimataifa.
Awali, Makamu wa Rais mara baada ya kufika eneo hilo, alitembelea maonesho ya wadau mbalimbali wa kiswahili ambao wamekuwa wakionesha kazi zao, ikiwemo kutoa mada na shuhuda za ukuaji wa lugha ya kiswahili.
Kauli mbiu ya maadhimisho ya siku hii ni ” kiswahili ni chachu ya maendeleo na utengamano duniani”
Akiongea katika maadhimisho hayo, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa amesema ukizungumza kiswahili unakuwa unaizungumzia historia ya Taifa la Tanzania, kutokana na Lugha hii kutumika katika Mapambano dhidi ya ukoloni na kuwaunganisha Watanzania.
Amesema, “Kipekee kabisa wizara inatambua mchango wa viongozi wote wa Serikali waliofanikisha kufanyika kwa tamasha hili la maadhimisho ya Siku ya Kiswahili Duniani”.
Mchengerwa ameongeza kuwa, Wizara yake itaendelea kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), ya mwaka 2022-2025 ya kuboresha Baraza la Kiswahili Tanzania (BAKITA), pamoja na kununua vifaa vya ukalimani ili kuweza kuikuza zaidi lugha hiyo Duniani.
“Kuanzia wiki ijayo sisi wizarani tumejipanga kufanya mijadala ya pamoja baina yetu na wenzetu UNESCO, ili kuona umuhimu wa umoja wa mataifa kuitumia Tanzania kwa ajili ya ujenzi wa chuo kikuu cha Kiswahili Duniani,” amesisitiza Waziti huyo.
Aidha, amebainisha kuwa katika kufanikisha Maadhimisho ya Siku ya Lugha ya kiswahili wamejadili mambo mbalimbali, ikiwemo matumizi ya Kiswahili Fasaha na Sanifu, ikiwemo fursa na faida zitokanazo na matumizi ya lugha hii katika Bara la Afrika”
Viongozi kadhaa wamehudhuria maadhimisho hayo, akiwemo Makamu Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Abrulhaman Omar Kinana, Waziri wa Utamaduni, Sanaa na Michezo, Mohamed Mchengerwa, Katibu Mkuu wa Wizara ya Utamaduni, Sanaa na Michezo, Dkt. Hassan Abasi, wadau mbalimbali na wananchi.