Serikali, imetoa siku kumi na nne kwa Mkurugenzi Mkuu wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bandari Tanzania (TPA), kuwasilisha ripoti ya vitu muhimu vinavyohitajika kwa maboresho ya miundombinu ya Bandari ya Bagamoyo.

Akizungumza mara baada ya ukaguzi wa Bandari hiyo Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete, amesema maboresho hayo yatarahisisha shughuli mbalimbali za kiuchumi na kukuza tato la Taifa.

“Kwa kuwa eneo hili la Bagamoyo ni muhimu sana kwa utalii nampa Mkurugenzi Mkuu wa TPA wiki mbili alete watalaam hapa waangalie vitu muhimu vya kuboresha”, amesema Mwakibete.

Mkurugenzi wa Halmashauri ya Bagamoyo, Shauri Selenda akifafanua jambo kuhusu utendaji wa soko la Bagamoyo, wakati Waziri huyo alipotembelea soko hilo mkoani Pwani.

Ameongeza kuwa, pamoja na maboresho ambayo Serikali imepanga kuyafanya bado inaendelea na mkakati wake wa kurasimisha Bandari bubu zinazozunguka eneo la Bahari ya Hindi ili kuweza kupunguza biashara za magendo.

Akiongea katika eneo hilo, Meneja Miliki wa TPA, Ndibalema Alexander amemuhakikishia Naibu Waziri kuwa watatuma watalaam wa kufanya tathmini ya mahitaji halisi ya maboresho ya miundombinu ya Bandari hiyo.

Awali, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Chalinze, Hassani Rajabu, aliishukuru Serikali kwa kutupia jicho Bandari ya Bagamoyo, na kusema maboresho ya miundombinu yatakayofanywa yataongeza pato kwa mkoa wa Pwani na Taifa zima kwa ujumla.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupeleke Mwakibete akizungumza na baadhi ya Wananchi wa Wilaya ya Chalinze Mkoani Pwani.  Kulia kwa Naibu Waziri Mwakibete ni Naibu Waziri wa Ardhi na Maendeleo ya Makazi na Mbunge wa Chalinze, Ridhiwani Kikwete.

Naibu Waziri wa Uchukuzi, Atupele Mwakibete yuko mkoani Pwani kwa ziara ya kikazi ya siku mbili, kukagua miradi mbalimbali mbalimbali inayosimamiwa na Wizara ya Ujenzi na Uchukuzi.

Mtibwa Sugar yabaki Ligi Kuu Bara, TZ Prisons kazi ngumu
Samia awapa pole waliovamiwa na Tembo