Waandishi wa vyombo vya Habari wa mitandao ya kijamii ikiwemo Blogs na Youtube, wametakiwa kufanya kazi kwa weledi na kuzingatia sheria na kanuni, na kuepuka upotoshaji unaofanywa na baadhi yao.

Meneja wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA), Kanda ya ziwa Mhandisi Francis Mihayo ameyasema hayo hii leo Julai 06, 2022 jijini Mwanza, wakati akifungua kikao kazi baina ya mamlaka hiyo na waandishi wa habari wa vyombo habari mtandaoni.

Amesema baada ya sekta ya Habari mtandaoni kukua, zimeibuka changamoto mbalimbali ikiwemo upotoshaji unaofanywa na baadhi ya luninga za mtandaoni ambapo kichwa cha habari kinakuwa hakina mahusiano na maudhui yaliyo ndani ya habari.

Meneja wa Mamlaka ya Mawasilino Tanzania (TCRA), Mhandisi Francis Mihayo akizungumza wakati wa ufunguzi wa kikao na Watoa huduma za maudhui kwa njia ya mtandao Kanda ya Ziwa kilichofanyika Julai 06, 2022 jijini Mwanza.

“Unakuta kichwa cha habari kimeandikwa ‘Imeisha Hiyo’ ukiingia ndani unakuta mwanzo hadi mwisho mtangazaji anasema na neno ‘Subcribe, bonyeza kengele’ kwa habari zaidi, sasa hiyo kwa wataalamu wenye leseni kutoka TCRA sitegemei muwe na kitu kama hicho” amesema Mihayo.

Awali, Mwenyekiti wa Chama cha Waandishi wa Habari Mkoa Mwanza, Edwin Soko amesema waandishi wanapaswa kuwa makini kwa kuimarisha ulinzi wa vifaa vyao mtandaoni ili kuepuka changamoto ya kudukuliwa.

Akiwasilisha mada kuhusu maadili ya uandishi wa habari, Mwenyekiti Mstaafu wa MPC, Deus Bugaywa amesema changamoto iliyopo kwenye vyombo vya mtandaoni ni kukosa dawati la uhariri wa zaidi ya mtu mmoja na hivyo kuwa na makosa mengi ya kimaadili.

Mwenyekiti Mstaafu wa Mwanza Press Club (MPC), Deus Bugaywa akiongea jambo wakati wa kutoa mada kuhusu maadili ya vyombo vya habari vya kimtandao.

Kwa upande wake Mwanasheria TCRA, Joseph Kavishe amesema ni kosa la jinai kuendesha mtandao wa kijamii bila kusajili hivyo kuwasihi wamiliki wa mitandao hiyo kufuata taratibu na kulinda utu wanapoandika habari.

Mamlaka ya TCRA Kanda ya Ziwa imetumia kikao hicho kutoa ufafanuzi wa mabadiliko madogo ya Kanuni za Maudhui Mtandao yaliyofanyika mwaka 2022 kwa lengo la kuboresha zile za awali zilizotoka kwa mara ya kwanza mwaka 2018.

Mabadiliko yaliyofanyika ni pamoja na kupuguza ada ya leseni kutoka shilingi milioni moja hadi shilingi laki tano kwa mwaka, na ada ya maombi kutoka shilingi laki moja hadi shilingi elfu hamsini, huku waandaaji wa maudhui yanayohusu michezo, sanaa, mapishi na elimu wakiwa hawatahitaji kuwa na leseni kutoka TCRA.

Mwanasheria  wa Mamlaka ya Mawasiliao Tanzania (TCRA), Joseph Kavishe akiongea wakati wa kikao na waandishi wa Habari juu ya kanuni za maudhui mtandaoni.

Nathaniel Chilambo anaswa Azam FC
Ahmed Ally ampigia kampeni Suma Mwaitenda