Ripoti mpya ya Umoja wa Mataifa (UN), inaonesha Idadi ya watu walioathiriwa na njaa duniani kupanda hadi kufikia watu milioni 828 mwaka 2021, ongezeko la takriban watu milioni 46 tangu 2020 na milioni 150 tangu kuzuka kwa janga la COVID-19.

Kulingana na ushahidi wa ripoti hiyo, kwasasa dunia inazidi kusonga mbali na lengo lake la kumaliza njaa, uhaba wa chakula na utapiamlo katika njia zake zote ifikapo mwaka 2030.

“Watu bilioni 2.3 duniani sawa na asilimia 29.3, walikuwa na uhaba wa chakula kwa wastani na kwa kiasi kikubwa mwaka wa 2021 ikilinganishwa na kabla ya kuzuka kwa janga hilo ambapo karibu watu milioni 924 walikabiliwa na uhaba wa chakula, ikiwa ni ongezeko la watu milioni 207 katika miaka miwili,” imesema.

Ukame uliotawala katika eneo ya nchi ya kusini mwa jangwa la Sahara.

Taarifa hiyo inasema, “Pengo la kijinsia katika uhaba wa chakula liliendelea kuongezeka mwaka wa 2021 – asilimia 31.9 ya wanawake duniani waliokuwa na uhaba wa chakula wa wastani au mbaya, ikilinganishwa na asilimia 27.6 ya wanaume ikiwa ni pengo la zaidi ya asilimia 4, ikilinganishwa na asilimia 3 mwaka wa 2020.”

“Takriban watu bilioni 3.1 hawakuweza kumudu lishe bora mwaka wa 2020, ikiwa ni ongezeko la milioni 112 kutoka mwaka wa 2019, jambo linaloakisi athari za mfumuko wa bei katika bei za vyakula vya walaji unaotokana na athari za kiuchumi za janga la COVID-19 na hatua zilizowekwa ili kuidhibiti,” iliongeza taarifa hiyo.

Aidha, watoto milioni 45 walio chini ya umri wa miaka mitano walikuwa wakikabiliwa na utapiamlo, ambao huongeza hatari ya vifo vya watoto kwa hadi mara 12 huku Watoto wengine milioni 149 walio chini ya umri wa miaka mitano walikuwa na ukuaji duni kutokana na ukosefu wa virutubishi muhimu katika lishe.

Moja kati ya sababu zinazotajwa kuchangia uharibifu wa mazingira na ukame ni pamoja na ukataji miti iliyo na matumizi mbalimbali kwa Wanadamu.

Toleo la 2022 la ripoti ya Hali ya Usalama wa Chakula na Lishe Duniani (SOFI), linawasilisha masasisho kuhusu usalama wa chakula na hali ya lishe duniani kote, ikiwa ni pamoja na makadirio ya hivi punde ya gharama na uwezo wa kumudu lishe bora.

Ripoti hiyo ni machapisho ya pamoja ya Shirika la Chakula na Kilimo (FAO), Mfuko wa Kimataifa wa Maendeleo ya Kilimo (IFAD), Mfuko wa Watoto wa Umoja wa Mataifa (UNICEF), Mpango wa Chakula wa Umoja wa Mataifa (WFP) na Shirika la Afya Duniani (WHO).

Hali ya ukame katika moja ya maeno nchini Tanzania

Simbachawene kuongoza harambee kampeni GGM KILI CHALLENGE 2022
Milioni wahudhuria ibada ya Hijja Mecca