Kocha Mkuu Mpya wa klabu ya Simba SC, Zoran Manoljović ameanza kutimiza jukumu ya kusuka kikosi kazi chake, tayari kwa maandalizi ya Msimu Mpya wa Ligi Kuu Tanzania Bara, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ pamoja na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Kocha Zoran aliyetangazwa kama Mrithi wa Kocha Franco Pablo Martin kutoka Hispania mwishoni mwa mwezi uliopita (Juni) amepanga kuanza na mpango wa kulisuka Benchi lake la Ufundi Simba, huku akimini wasaidizi atakaokuwa nao watawezesha lengo linalokusdiwa klabuni hapo.
Uongozi wa Simba SC ulimpa makali yote Kocha huyo kutoka nchini Serbia ya kufanya maamuzi katika Benchi lake la Ufundi kwa kutafuta wasaidizi wawili atakaokwenda nao kwenye Kambi ya timu hiyo itakayokuwa Misri kuanzia Julai 15 kwa maandalizi ya msimu mpya (Pre-Season).
Katika kuhakikisha Simba SC inakuwa na Benchi la ufundi imara, Zoran anatakiwa kutua Misri akiwa na wasaidizi wake wawili ambao ni kocha wa Makipa pamoja na wa Viungo.
Simba SC kwa sasa haina kocha wa Makipa baada ya kuachana na Tyron Damons aliyepata kibarua kingine Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini, huku pia ikiachana na kocha wa Viungo, Mhispania Daniel De Castro.
Taarifa kutoka ndani ya Klabu ya Simba SC zinaeleza kuwa, tayari Kocha Zoran ana majina mawili ya makocha atakaoenda nao kambini mmoja akiwa ni kocha wa makipa Mohamed Haniched aliyewahi kufundisha USM Blida, USM EL Harrach na USM Alger ambazo zote zinatoka nchini kwao Algeria.
Kwa upande wa Kocha wa Viungo, jina la Kareem Bayey linatajwa sana kutokana na ukaribu uliopo kati ya Kocha Zoran na Kocha huyo wa Viungo ambaye anaelezwa amekuwa naye kwenye timu nyingi alizofundisha huko nyuma.
Zoran inaelezwa anavutiwa zaidi na kocha huyo wa viungo kwani mbali ya uwezo wake huo amekuwa pia akimsaidia kama kocha msaidizi ndio maana kila anapokwenda kufundisha anakuwa pamoja naye.
Mabosi wa Simba wamekubaliana na mapendekezo ya wasaidizi hao wa Zoran atakaokuwa nao kwenye kambi ya timu hiyo Misri.
Simba SC inaendelea kusuka kikosi matata kabisa, huku ikiwatambulisha wachezaji wanne hadi sasa ambao ni Moses Phiri (Zambia), Victor Akpan (Nigeria), Habib Kyombo na Nassoro Kapama (Tanzania).
Wengine wanaotajwa huenda wakajiunga na kikosi cha Simba SC katika kipindi hiki cha usajili ni Cecar Lobi Manzoki (Jamhuri ya Afrika ya Kati), Nelson Okwa (Nigeria) na Augustine Okra (Ghana).