Wadaiwa sugu, wamesamehewa riba ya kodi ya pango la ardhi kwa masharti ya kulipa madeni yao ya msingi ndani ya miezi sita kuanzia Julai hadi Desemba 2022.
Waziri wa Ardhi Nyumba na Maendeleo ya Makazi Dkt Angeline Mabula amesema msamaha huo umeridhiwa na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan.
Katika mkutano wake na wananchi wa kijiji cha Nyachoka kilichopo Wilayani Serengeti mkoani Mara wakati wa zoezi la kukabidhi hati miliki za kimila, Waziri Mabula amesema jumla ya hatimiliki za kimila 6,155 zimekamilika na kutolewa kwa wananchi wa vijiji 22 katika wilaya ya Serengeti.
“Kati ya hati hizi 6,155 hati 1621 sawa na asilimia 26 zimekamilika kwa ajili ya akina mama na hatimiliki 1,519 sawa na asilimia 25 ni za umiliki pacha kati ya Wanaume na Wanawake,” amesema Dkt. Mabula.
Dkt Mabula amesema, “Kuna wengi wanadaiwa madeni ya muda mrefu kwa hiyo kumetokea msamaha kuanzia mwezi julai mpaka Desemba mwaka huu na watalipa ndani ya miezi hii sita, wale ambao madeni yao yana miaka mitano kurudi nyuma watalipa bila ile tozo ya riba,” amefafanua Waziri..
Ameongeza kuwa Rais Samia ameridhia msamaha huo kupitia Waziri wa Fedha kwa kushirikiana na Waziri wa Ardhi baada ya kuweka utaratibu mzuri kuondolewa tozo ya msamaha huo wa miezi sita pekee.
“Sasa kama una ndugu mpigie simu mwambie Serikali imetoa msamaha kwa wadiwa sugu ili watoke katika jina baya la wadaiwa sugu kwenda kulipa madeni bila riba” amesisitiza Wziri huyo.
Kuhusu hatua ya kumilikishwa ardhi kwa nyaraka, Dkt. Mabula amesema ipo faida ambazo ni pamoja na usalama wa ardhi, uhakika wa milki, kupunguza migogoro pamoja na nyaraka hiyo kutumika kama dhamana.
Zaidi ya wananchi 6,000 katika vijiji 22 Mkoani Mara, wamepangiwa matumizi bora ya ardhi katika maneo yao na kuwekewa mipaka ya kudumu ili kuepuka migogoro ya ardhi.