Meneja wa Habari na Mawasiliano wa Simba SC Ahmed Ally amesema klabu hiyo inajiandaa kumtambulisha mchezaji mwingine wa Kimataifa miongoni mwa wachezaji watatu waliosajilia katika orodha yao ya usajili wa msimu wa 2022/23.

Simba SC imejizatiti kuboresha kikosi chake kwa kufanya usajili, baada ya kuambulia patupu msimu uliopita kwa kuutema Ubingwa wa Ligi Kuu na Kombe la Shirikishiri Tanzania Bara ‘ASFC’ huku ikishia hatua ya Robo Fainali Kombe la Shirikisho Barani Afrika kwa kutolewa na Orlando Pirates ya Afrika Kusini.

Ahmed amesema wamejiandaa kuendelea kuwafurahisha Mashabiki na Wanachama wa Simba SC kwa kutangaza wachezaji wengine watatu, baada ya kufanya hivyo jana Jumatano (Julai 13) kwa Kiungo Kutoka nchini Ghana Augustine Okrah.

“Kwa hakika jana Mashabiki na Wanachama wetu wamefurahi sana baada ya kumtambulisha kwao Okrah, nilipokea simu nyingi na ujumbe mfupi kutoka kwa watu mbalimbali wakithibitisha furaha yao, kufuatia usajili wa mchezaji huyu,”

“Pia nimepokea ujumbe kutoka kwa Waandishi wengi wa Ghana wakitupongeza kwa kumsajili Okrah, hii kwangu imenidhihirishia kwamba, tayari Vyombo vya Habari vya Ghana vimeanza kumfuatilia mchezaji huyu, na pia vitaifuatilia Ligi yetu msimu ujao,”

“Ninawaambia bado wengine watatu ambao tutawatambulisha wakati wowote kuanzia sasa, Simba SC ya msimu ujao itatisha sana, tunasubiri muda wa kuanza msimu ili kudhihirisha dhamira yetu ya kurejesha heshima ndani ya Tanzania, na upande wa Kimataifa tutapambana kufikia lengo letu kucheza Nusu Fainali.” Amesema Ahmed Ally

Hadi sasa Simba SC imeshawatambulisha wachezaji watano ambao ni Moses Phiri (Zambia), Victor Akpan (Nigeria), Augustine Okrah (Ghana), Nassoro Kapama na Habib Kyombo (Tanzania).

Watatu washikiliwa vifo vya vijana 21 kwenye baa
Mvutano waibuka eneo la kumuhifadhi Rais wa zamani Angola