Kikosi cha Simba SC kimewasili salama mjini Ismailia-Misri tayari kwa Kambi ya kujiandaa na msimu mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Simba SC iliyoanza safari jana Alkhamis (Julai 14) Mchana kupitia Ethiopia, imewasili mjini Ismailia-Misri leo Ijumaa (Julai 15) Alfajiri, na baadae itaanza maandalizi chini ya Kocha Mkuu Zoran Maki kwa usaidizi wa Kocha mzawa Seleman Matola.
Baada ya kuwasili mjini humo, Kocha Maki amesema anaamini muda wa majuma matatu utatosha kuwaandaa vyema wachezaji wake kuelekea mchezo wa Ngao ya Jamii na Michuano mingine ya msimu mpya wa 2022/23.
“Tumefika salama, mazingira ya hapa ni mzuri yatafaa kuwaandaa vyema wachezaji wangu katika kiwango cha hali ya juu, muda wa majuma matatu utatosha kabisa kuwa na maandalizi mazuri,”
“Nitakua na wakati mzuri wa kuendelea kuwatambua vizuri wachezaji wangu nikiwa hapa, nilianza kuwafuatilia kwa Video tangu nilipotangazwa kuwa Kocha Mkuu Simba SC, sasa ni wakati wa kufanya kazi kwa vitendo.” amesema Kocha huyo kutoka nchini Serbia
Hata hivyo Simba SC inaanza maandalizi ya msimu mpya ikiwakosa wachezaji wake watano waliobaki Dar es salaam kwa majukumu ya Timu ya Taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’.
Wachezaji waliobaki Dar es salaam ni Mlinda Lango Aishi Manula, Mabeki wa Pembeni Shomari Kapombe, Mohamed Hussein, Kiungo Mazamiru Yassin na Mshambuliaji Kibu Denis.
Taifa Stars inakabiliwa na mchezo wa kuwania kufuzu Fainali za Mataifa Bingwa Barani Afrika ‘CHAN 2022’ zitakazounguruma Algeria baadae mwaka huu, dhidi ya Somalia.