Hatimaye Klabu ya Geita Gold FC ipo huru kufanya usajili wa Wachezaji kuelekea msimu Mpya wa Ligi Kuu, Kombe la Shirikisho ‘ASFC’ na Michuano ya Kimataifa inayoratibiwa na Shirikisho la Soka Barani Afrika ‘CAF’.
Geita Gold FC itashiriki Michuano ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, kufuatia Tanzania kuwa na nafasi nne kwenye michuano ya Kimataifa msimu ujoa, huku timu hiyo ikimaliza nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu msimu ujao.
Afisa Mtendaji Mkuu wa Geita Gold FC Simon Shija amethibitisha kuwa huru kwa Klabu yao katika Usajili, baada ya kukamilisha taratibu zote za kumlipa stahiki aliyekua Kocha wa kikosi chao Etienne Ndayiragije.
Juni 25, mwaka huu FIFA iliifungia timu hiyo kusajili hadi itakapomlipa aliyekuwa Kocha wake, Ettiene Ndayiragije ambaye alifungua madai akidai fidia ya kuvunjiwa mkataba na malipo mengine wakati akiifundisha timu hiyo.
Shija amesema klabu yao imetekeleza matakwa yote ya kisheria na kikanuni kwa kuzingatia miongozo ya shirikisho hilo na sasa ipo huru kuendelea na utendaji wake.
“Uongozi wa klabu ya Geita Gold FC unapenda kuwataarifu mashabiki, wadau na wapenda michezo kuwa imemalizana na adhabu ya FIFA iliyokuwa na zuio la kuifungia kufanya usajili,”
“Tunaomba wadau kuendelea kushirikiana na klabu na milango ya udhamini ipo wazi, klabu imepanga kufanya vizuri msimu ujao ili kuendeleza hali ya ushindani katika michuano ya ndani na kimataifa,” amesema Shija.
Kabla ya taarifa hiyo, Geita Gold ilikuwa haijaanza kufanya usajili wala kutambulisha mchezaji yeyote kuelekea msimu mpya huku kukiwa na ukimya mkubwa, lakini baada ya taarifa hiyo vigogo hao wameanza mikwara wakitajwa kumalizana na Ramadhan Chombo na baadhi ya nyota wengine.