Serikali imeagiza Wakala wa barabara mjini na Vijijini (TARURA), Mkoa wa Singida kuvunja mkataba baina yao na Mkandarasi wa Kampuni ya Bullem Investment limited, wanaojenga Barabara ya kutoka Kitongoji cha Majengo hadi Hospitali ya wilaya kutokana na kushindwa kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Agizo hilo limetolewa na Waziri Mkuu Kassimu Majaliwa Wilayani Manyoni, baada ya kupata malalamiko ya wananchi wa maeneo hayo waliomueleza kushindwa kukamilika kwa Barabara hiyo kwa kipindi kirefu na kusababisha usumbufu kwa wakazi wa eneo hilo.
Waziri Mkuu pia, amemuagiza Meneja TARURA Mkoa wa Singida kukagua na kumlipa Mkandarasi kulingana na asilimia zilizofikiwa katika Ujenzi wa Barabara hiyo, na asilimia zilizobaki apatiwe Makandarasi mwingine atakayeweza kukamilisha kazi hiyo kwa wakati.
Aidha, kutokana na kutokamilika kwa miradi mbalimbali Wilayani Manyoni ikiwemo mpango wa wamachinga, ujenzi wa soko na kutosikiliza na kutatua changamoto za wakazi, Waziri Mkuu amewahakikishi wananchi hao kuwa viongozi walihusika kukwamisha miradi ya Serikali watachukuliwa hatua za kinidhamu.
Wananchi hao, pia walilalamikia kutozwa fedha wakati wa kujifungua kina mama wajawazito, ukosefu wa masoko na huduma isiyoridhisha wa stendi ya mabasi na madeni ya fidia ya ardhi ya wananchi kitu ambacho kinawapa wakati mgumu.
Hata hivyo Waziri Mkuu amewaahidi wananchi hao kushughulikia suala la madeni ya fidia za ardhi, pamoja na changamoto ya Kodi huku akimtaka Mkuu wa Mkoa wa Singida, Bilinith Mahenge kuhakikisha anarudi kuwasikiliza wafanyabiashara wadogo na kutatua changamoto zinazowakabili.