Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri, Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako amekutana na baadhi ya Wazee wastaafu wa mifuko ya PSSSF na NSSF na kusikiliza changamoto zinazowakabili.

Waziri Profesa Ndalichako alisema kupitia mkutano huo wataendelea kujifunza na kutatua kero mbalimbali zinazowakabili wastaafu hivyo aliwaomba watendaji wa mifuko hiyo kuweka utaratibu wakusikiliza kero na kuzipatia ufumbuzi.

“Nimeona nitenge muda kusikiliza changamoto walizonazo wastaafu wa NSSF na PSSSF hivyo zile changamoto ambazo tunaweza kuzitatua papo kwa papo tunafanya hivyo na zile ambazo zinahitaji muda tunachukua vielelezo na kuzifanyia kazi,” amesema Prof. Ndalichako.

Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri, Mkuu, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu, Profesa Joyce Ndalichako

Amesema, “Ni jukumu na ni wajibu wa kila mtumishi wa umma kusikiliza na kuzipatia ufumbuzi kero mbalimbali za wananchi wakiwemo wanachama wa Mifuko ya Hifadhi ya jamii.”

Amesema, lengo la Serikali kupitia Mifuko ya Hifadhi ya Jamii ni kuhakikisha wanatoa huduma kwa wastaafu bila usumbufu wowote na kuwahudumia kwa wakati na kwa kiwango kinachotakiwa kwa mujibu wa sheria na kanuni zinazoongoza Mifuko ya Hifadhi ya Jamii.

Naye, Mzee Ramadhani Abdallah ambaye ni mstaafu wa Jeshi la Magereza Tanzania Bara, alipongeza kazi kubwa inayofanywa na Waziri Profesa Ndalichako ya kusikiliza na kutatua kero mbalimbali za wastaafu hatua ambayo itapunguza changamoto za wastaafu.

Prof. Joyce Ndalichako akiongea na mmoja wa Wazee hao.

Mkutano huo uliohudhuriwa na Mkurugenzi Mkuu wa NSSF, Masha Mshomba na Mkurugenzi Mkuu wa PSSSF, CPA Hosea Kashimba pamoja na watendaji wa mifuko hiyo na Ofisi ya Waziri Mkuu.

Kamati kufuatilia utendaji wa majeshi kuundwa
IGP Wambura, Balozi Sirro waapa Ikulu