Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amesema ataunda kamati ya watu 12 na sekretarieti ya watu watano kwa ajili ya kufuatilia utendaji kazi wa vyombo vya ulinzi na usalama nchini.
Kauli hiyo, imetolewa na Rais Samia mara baada ya kumuapisha Camillus Wambura kuwa Inspekta Jenerali wa Polisi (IGP), Ikulu ya Chamwino jijini Dodoma hii leo Julai 20, 2022.
Amesema, kamati hiyo itakayooongozwa na Jaji Mkuu mstaafu Othumani Chande, na makamu wake atakuwa aliyewahi kuwa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi Ombeni Sefue na itakuwa ikimshauri njia bora ya kuleta mabadiliko ya utendaji kwenye matokeo chanya.
“Tutaanza na polisi, wakimaliza wakileta ripoti tutafanya marekebisho, tunakwenda majeshi mengine, tunakwenda magereza, hivyo mpaka tumalize ili kupata utendaji ulio bora na tutakuja na miundo inayofaa sasa hivi ili kuwa na jeshi linalofaa na bora,” amefafanua Rais Samia.
Wengine walioapishwa ni, aliyekuwa IGP Simon Sirro kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zimbabwe, Luteni Jenerali, Mathew Mkingule kuwa Balozi wa Tanzania nchini Zambia na Dkt. Suleiman Haji Suleiman kuwa Balozi.
Mkuu huyo mpya wa Jeshi la Polisi, IGP Wambura kabla ya kuteuliwa kushika nyadhifa hiyo alikuwa ni Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) nafasi ambayo kwasasa inashikiliwa na Ramadhan Kingai aliyeteuliwa na kuapishwa hii leo ambapo awali alikuwa Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Kigoma.