Rais wa Mabingwa wa Soka Tanzania Bara Young Africans Hersi Said kwa kushirikiana na Kamati ya Utendaji ya klabu hiyo, ameunda Kamati ya Mashindano yenye watu wanane.

Kamati hiyo ambayo imeanza kazi rasmi leo Jumatano (Agosti 10) itaongozwa na Mwenyekiti Rodgers Gumbo ambaye ni Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya Young Africans.
Wajumbe wa kamati hiyo ni Mustapha Himba, Lucas Mashauri, Seif Ahmed (Magari), Pelegrinus Rutayuga, Davis Mosha na Majid Suleiman.

Maamuzi ya kuundwa kwa Kamati hiyo yameafikiwa siku chache kabla ya kikosi cha Mabingwa hao wa Tanzania Bara kupambana na Simba SC katika mchezo wa Ngao ya Jamii, Jumamosi (Agosti 13) Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam.

Pia kamati hiyo imetajwa siku moja baada ya Young Africans kumfahamu mpinzani wake kwenye michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika.

Young Africans wataanza kupambana na Mabingwa wa Sudan Kusini ‘Zalan FC Rumbek’ ambao wataanzia nyumbani kisha watamaliza jijini Dar es salaam, Uwanja wa Benjamin Mkapa.

Endapo Young Africans akifanikiwa kupita katika hatua hiyo ya awali, atakutana na mshindi kati ya St George ya Ethiopia dhidi ya Al Hilal ya Sudan.

Juma Kaseja, KMC njia panda
Raila aongoza kwa kura Kigali