Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan ameridhia tarehe 23 Agosti 2022 iwe siku ya mapumziko, ili Watanzania wawepo majumbani na waweze kuwapokea makarani wa sensa na kutoa maelezo sahihi.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa amesema hayo Kwenye Kikao cha Kamati ya Kitaifa ya Sensa, Agosti 18, 2022, katika Ukumbi wa Mikutano wa Kimataifa wa Julius Nyerere, Dar es Salaam.
Sensa ya watu na Makazi, inatarajiwa kufanyika tarehe 23 Agosti kuanzia Saa 6 usiku wa siku hiyo na kuendelea mpaka zoezi litakapokamilika.
Taarifa zitakazokusanywa katika Dodoso la Jamii Tarehe 21 na 22 Agosti 2022, zitahusu huduma za jamii kama elimu, afya, maji, barabara, masoko, huduma za fedha, majosho na miundombinu.
Baadhi ya maswali, yatakayoulizwa na Karani wa Sensa yanahusu kama mwanakaya ana Cheti cha Kuzaliwa au Tangazo la Uzazi, Hati ya Kusafiria, Bima ya Afya NHIF/CHF na bima nyingine za afya.