Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena amesema Sheria ya Vyombo vya Habari ya Mwaka 2016, ilikataliwa siku ya kwanza baada ya kusainiwa na kuanza kutumika kama mwongozo kwa vyombo vya habari nchini.

Meena, ameyasema hayo Agosti 17, 2022 wakati akifanya mahojiano na vyombo mbalimbali vya Habari jijini Dodoma, na kudai kuwa Wanahabari walianza kudai mabadiliko ya sheria za habari mapema, kwa kuwa sheria zilizopitishwa mwaka 2016 hawakuridhika nazo.

Amesema, “Sheria ya Habari ya Mwaka 2016 ilipitishwa katika mazingira ambayo sisi wadau wa habari hatukuridhika, maeneo mengi ya msingi ambayo tuliyataka yawe sehemu ya sheria hiyo yaliachwa.”

Mjumbe wa Kamati Tendaji ya Jukwaa la Wahariri Tanzania (TEF), Neville Meena katika mahojiano juu ya Mabadiliko ya Sheria ya Habari aliyoyafanya na chombo kimoja cha Habari jijini Dodoma Agosti 17, 2022.

Aidha, Meena ameongeza kuwa baada ya sheria hiyo kupita, wadau wa habari walikutana, na kujadili mchakato wa kutaka mabadiliko ya sheria hizo ingawa mjadala wao haukuwa na nguvu.

Ameongeza kuwa, Wadau wa habari waliamini vyombo vya habari vitazidi kusinyaa kutokana na yale yaliyomo ndani ya sheria hizo, na kwamba licha ya kudai mabadiliko hayo katika utawala uliopita bado hawakuona juhudi zozote zilizofanywa na Serikali.

‘‘Wadau wa habari wakiwemo UTPC, TAMWA, MISA-TAN, LHRC, TLS, Twawezaa, Sikika, THRDC na wengine, walikaa pamoja na kuangalia madhara yanayoweza kutokea kutokana na sheria hiyo, lakini tangu wakati huo hakuna dalili chanya za kufanyiwa kazi,” amefafanua Meena.

Hata hivyo, amebainisha kuwa “Utawala huu (wa Rais Samia Suluhu Hassan), umeonesha nia toka mwanzo ya kulishughulikia hili, na ndio maana hata vyombo vya habari vilivyofungiwa Rais alivifungua na tunaiona dhamira ya kweli na tuna imani tutafikia muafaka hata kama sio kwa asilimia 100,” amebainisha Meena.

Baada ya serikali, kuona umuhimu wa kupitia sheria hizo iliandaa maboresho na kupeleka kwa wadau ili wayapitie na kupata mapendekezo ambayo yanapendekeza vifungu vilivyo na mapungufu au hatari kwa wanahabari katika kutekeleza majukumu yao.

Pamoja na mambo mengine, eneo jingine lenye ukakasi ni la matangazo ya Serikali kuratibiwa na Mkurugenzi wa Idara ya Habari Maelezo na usajili wa magazeti wa kila mwaka tofauti na ule wa awali wa kudumu.

Waziri Mkuu atatua mgogoro wa ardhi uliodumu miaka 3
Wandimba: Hakuna jipya kwa Simba SC