Kamishna Mkuu wa shirika la Umoja wa Mataifa la kuhudumia wakimbizi (UNHCR), Filippo Grandi amewahimiza wahisani kuunga mkono suluhuhisho la uhudumiaji wa wakimbizi, na kusifu maendeleo yaliyopigwa katika ulinzi dhidi yao nchini Tanzania.
Grandi, ameyasema hayo wakati akihitimisha ziara yake ya siku tatu nchini hapa na kusema miongoni mwa suluhu hizo ni pamoja na hatua endelevu ya wakimbizi kurudi nyumbani kwa hiari, ambapo pia alijadiliana na Serikali umuhimu wa kuweka mazingira rafiki ya kurejea kwa wakimbizi katika nchi zao.
Amesema, anaipongeza Tanzania na wananchi wake kwa historia yao ya muda mrefu ya kuwapokea na kuwahifadhi wakimbizi, pamoja na juhudi za kuendeleza ulinzi na suluhisho kwa jamii hiyo kwa kuzingatia mkataba wa kimataifa wa wakimbizi.
Amesema, “Kwa kweli nimetiwa moyo na juhudi za serikali za kuimarisha ulinzi wa wakimbizi, na kusimama pamoja nao na ahadi ya UNHCR ya kuunga mkono Tanzania na kulinda haki za wakimbizi wanaohifadhiwa hapa bado ni thabiti.”
Hata hivyo, amesema amefurahishwa zaidi kuona juhudi za Serikali ya Tanzania za kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa watoto wakimbizi, akisema hatua hiyo itawapa ulinzi muhimu wa kisheria na kupunguza hatari ya kutokuwa na utaifa hasa kwa kutoa aina ya utambulisho pale wanaporejea katika nchi zao.
Kwa sasa, Tanzania inahifadhi zaidi ya wakimbizi 248,000, hasa kutoka nchini Burundi na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC), na wengi wao wanaishi katika kambi za Nduta na Nyarugusu zilizopo mkoani Kigoma huku wakimbizi 142,000 wa Burundi wakirejea makwao kwa hiari tangu Septemba 2017.
Ziara ya Grandi nchini hapa, Tanzania inafuatia mazungumzo ya ngazi ya juu yaliyoitishwa na serikali ya Tanzania na UNHCR mwezi Machi 2022 ili kukubaliana kuhusu hatua za kuimarisha ulinzi na ufumbuzi wa chngamoto za wakimbizi.