Waathirika wa ugonjwa wa Trakoma wamehimizwa kujitokeza kuitafuta matibabu kwa sababu ugonjwa huo unatibika kwa njia ya Upasuaji.
Rai hiyo imetolewa hivi karibuni jijini Dar es Salaam na Mkurugenzi Mkuu wa Shirika lisilo la kiserikali la SightSavers Tanzania, Godwin Kabalika alipozungumza na waandishi wa habari kwenye mkutano ulioandaliwa na Wizara ya Afya uliojikita kujadili kuhusu magonjwa yasiyopewa kipaumbele
Kabalika amesema mgonjwa anapofanyiwa upasuaji hatua hiyo humuondoa katika uwezekano wa kupata upofu wa kudumu unaoweza kujitokeza kutokana na athari za ugonjwa huo.
“Shirika letu tumeweza kuisaidia Wizara ya Afya katika mikoa mitano Ruvuma, Lindi, Morogoro, Singida, na Manyara na mafanikio makubwa tuliyoona ni kwamba tumeweza kusaidia watu mbalimbali ambao waligundulika wana ugonjwa wa vikope (Trakoma),” alisema Kabalika.
“Kikubwa tunajivunia wanaweza kufanya shughuli zao vizuri kama binadamu wengine na wanaweza kuchangia kwenye maendeleo, kujikwamua kwenye familia na kwenye jamii,”
Kabalika ameongeza kuwa bado zipo imani potofu kwenye jamii kuhusu ugonjwa na kwamba Shirika hilo kupitia watoa huduma za afya ngazi ya jamii limekuwa likiendelea kuelimisha jamii.
SightSavers Tanzania, limekuwa likifanya shughuli zake nchini tangu miaka ya 70 kwa ushirikiano wa karibu na Serikali kupitia Wizara ya Afya kwa kujikita kufanya elimu jumuishi ya masuala ya afya ya macho na ya watu wenye ulemavu.