Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan amelitaka Jeshi la Polisi nchini kutenda haki katika kazi zake za kila siku, ikiwemo kuwa makini hasa Viongozi wa ngazi ya juu ili kuleta uwiano wa utendaji kazi kwa askari wadogo.

Samia ametoa wito huo hii leo Agosti 30, 2022 wakati akifungua kikao cha maofisa wa Polisi Makao Makuu, Makamanda wa Mikoa na Vikosi, kilichofanyika katika Shule ya Polisi Moshi, Kilimanjaro.

Amesema, ni wazi kuwa uharibifu kiutendaji unaanzia ngazi ya juu, na kwamba suala la ubambikiaji wa kesi limekuwa ni tatizo na huenda linasababishwa na watu wanaokamatwa kushindwa kutoa hongo kwa Askari.

“Nimesikia hapa kuna msamaha wa kesi chungu mzima, sasa kesi hizi naambiwa zilikosa ushahidi wa kutosha hii ina maana waliokamatwa huenda walikataa kutoa kitu kidogo kwa Askari nendeni mkarekebishe hili Makamanda wa Mikoa” amefafanua Rais Samia.

Ameongeza kuwa, “Kule kwetu sokoni tunaita Marikiti, sasa huwa tunanunua samaki na ili kumkagua kama ni mzima huwa tunaangalia mashavu yakiwa yameharibika na mkia upo legelege basi tunajua hafai na mpaka mashavu yameharibika ni lazima shida ilianzia kichwani.”

Rais Samia ameendelea kufafanua kuwa, “Kama shida inaanzia kichwani basi ni hivyo na katika Jeshi la Polisi tatizo lipo juu, na hawa Askari wetu wa chini wanaiga huko naomba tubadilishe hili na tulifanyie kazi.”

Katika hatua nyingine Rais Samia pia amelionya Jeshi la Polisi nchini kuacha kutumia wadhamini kufanya vikao kazi bali wajitahidi kufanya wao kwani suala hilo linatoa mwanya wa kushindwa kuchukua hatua za kinidhamu pindi wadhamini hao wanapokiuka sheria.

Amesema, kikao kilichofanyika hii leo kimedhaminiwa na taasisi mbalimbali ambazo zinaongozwa na binadamu wenye uwezo wa kufanya makosa hivyo kitendo hicho kinaweza kusababisha kushindwa kutoa adhabu stahiki kwa wahusika pale wanapofanya makosa.

Serikali: Trakoma inatibika, 'jitokezeni'
Kenya: Mahakama yaainisha hatua tisa zuio la urais wa Ruto