Licha ya Kutwaa Ubingwa wa Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati ‘CECAFA’ na kupata nafasi ya kushiriki Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika 2022, Kocha Mkuu wa Simba Queens Sebastian Nkoma amesema bado ana kazi kubwa ya kufanya ili kuhakikisha timu inafanya vizuri kwenye michuano hiyo.
Simba Queens itashiriki michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika itakayoshirikisha timu nane kutoka Barani humo, mwezi Septemba mwaka huu nchini Morocco, itakayoshirikisha wakiwamo mabingwa watetezi Mamelodi na mwenyeji Far Rabat.
Wekundu hao ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake (WPL) kwa misimu mitatu mfululizo, waliweka heshima na kuandika rekodi ya kuwa timu ya kwanza Tanzania kutwaa taji la ‘CECACA’ baada ya kuifunga She Corporates ya Uganda, Jumamosi (Agosti 27) bao 1-0, Uwanja wa Azam Complex Chamazi jijini Dar es salaam.
Kocha Nkoma amesema amefurahishwa kutwaa taji hilo na kuwa miongoni mwa timu zilizoleta msisimko wa Soka, lakini bado ana kazi kubwa ya kufanya kutokana na upungufu aliouona.
“Yalikuwa mashindano mazuri kwetu, yametujengea kujiamini na yametoa kipimo kikubwa kuelekea mashindano ya kimataifa. Nina kazi ya kufanya kwa sabau kuna upungufu nimeuona,” amesema kocha huyo mzawa.
“Nina muda wa kutosha kabla ya kwenda Morocco. Nitahakikisha nasawazisha makosa yaliyojitokeza kwa lengo la kuendeleza ubora hadi kwenye mashindano makubwa tunayokwenda kushiriki.”
Wakati kocha huyo akifunguka hayo, kocha wa zamani wa Simba Queens, Matty Diola amewapongeza wachezaji na Benchi la Ufundi, huku akisema kuwa ni mwanzo mzuri kuelekea kwenye mashindano makubwa yaliyo mbele yao.
“Kupata michezo ya kimataifa ya mashindano kumewajengea uzoefu na ukomavu kuelekea michuano mikubwa iliyo mbele yao. Nina imani kubwa na kocha pamoja na wachezaji na natarajia mwendelezo mzuri kuelekea mashindano hayo,”
“Kupitia mashindano hayo kuna kitu kimeongezeka kwa wachezaji na kwa upande wa kocha. Naamini kuna ubora na upungufu kauona akiufanyia kazi timu inaweza kuiwakilisha nchi vizuri na kufika mbali.” amesema Matty Diola.