Kiungo Mshambuliaji kutoka nchini Ghana Bernard Morrison, ameongezea Dozi ya mazoezi kwenye kikosi cha Mabingwa wa Soka Tanzania Bara, ili azidi kuimarika kwa ajili ya kujiandaa na michezo mbalimbali ya Ligi Kuu Tanzania Bara na Michuano ya Kimataifa ya Ligi ya Mabingwa Afrika.

Morrison aliyejiunga na Young Africans akitokea Simba SC, ameongezewa Dozi hiyo, zikisalia siku chake kabla ya mchezo wa Ligi Kuu dhidi ya Azam FC utakaounguruma Septemba 6, Uwanja wa Benjamin Mkapa na Septemba 11 itawavaa Mabingwa wa Sudan Kusini Zalan FC katika Michuano ya Ligi ya Mabingwa Barani Afrika jijini Dar es Salaam.

Kocha Mkuu wa Young Africans Nasredeen Nabi amesema hana Presha na michezo hiyo miwili dhidi ya Zalan FC kwa sababu kikosi chake kina nafasi nzuri ya kusonga mbele ukilinganisha na wapinzani wao.

Nabi amesema, wachezaji wake wana nguvu na wako tayari kwa kupambana dhidi ya wageni hao ambao wameomba kutumia Uwanja wa Benjamin Mkapa kama nyumbani kwao.

Ameongeza, ana imani na kikosi chake lakini ameamua kumwongezea mazoezi Morrison ili afikie kiwango anachokihitaji kabla ya kuwavaa Zalan.

“Kulingana na ubora wa kikosi changu, nimeona nimpe Morrison (Bernard) mazoezi mengine tofauti ili kuwa imara zaidi na tayari kwa asilimia zote kwa sababu nina imani kubwa ya kufanya vizuri dhidi ya Zalan FC ili nitinge hatua inayofuata,” amesema Nabi.

Ameongeza presha ya benchi lake la ufundi iko kwa Morrison ambaye kwa sasa anasimamiwa mazoezi na, Healmy Gueldich ambaye amemtengenezea programu maalum winga huyo.

“Tunahitaji kuwa na mawinga walio tayari kiushindani kabla ya kuingia katika hatua ya pili ya mtoano, tatizo Morrison bado hajawa katika kiwango bora ambacho tunakitaka, ndio maana tunamjenga zaidi,” amesema Nabi.

Amesema, anatambua kama Morrison akiwa fiti kwa asilimia kubwa jinsi alivyo hatari, anaamini anaweza kuongeza kitu kwa kushirikiana na wengine wakiwako, Fiston Mayele na Stephan Aziz Ki.

Young Africans yang'atwa sikio Afrika
Waasi wa zamani wala kiapo chini ya ulinzi mkali