Mshambuliaji kutoka nchini Zimbabwe na klabu ya Azam FC Prince Dube amesema yupo tayati kuikabili Young Africans katika mchezo wa Mzunguuko watatu wa Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu 2022/23.
Azam FC itakua mgeni wa Young Africans Jumanne (Septemb 06), katika Uwanja Benjamin Mkapa jijini Dar es salaam, huku timu hizo zikiwa na mtazamo wa kiushindani kutokana na kuwa na vikosi vyenye ubora.
Dube ambaye aliifunga Young Africans msimu wa 2020/21 Uwanja wa Benjamin Mkapa, amesema yupo FIT kwa ajili ya mchezo wa Jumanne, hivyo endapo atapewa nafasi ya kwa sehemu ya kikosi atapambana na kuhakikisha anaisaidia timu yake kuzinyakua alama tatu muhimu.
Amesema siku zote Young Africans inapokutana na Azam FC mchezo huwa na upinzani mkali, na kwa bahati mbaya msimu uliopita hawakufanikiwa kupata matokeo mazuri dhidi ya Wakongwe hao kutoka Jangwani-Dar es salaam.
“Mara kadhaa tulizokutana na Young Africans mchezo unakua mgumu na ushindani mkubwa, tunawaheshimu kama miongoni mwa timu kubwa katika ligi ya Tanzania Bara.”
“Naamini mchezo ujao utakuwa na ugumu wake, Young Africans wana malengo yao na sisi kama Azam FC tuna malengo yetu, hivyo mchezo utakuwa mgumu, lakini kila mmoja amejipanga kivyake kuhakikisha anashinda.”
“Msimu uliopita sikuwa sehemu ya kikosi cha Azam FC kwa sababu nilikuwa majeruhi, lakini ninashukuru mchezo huu wa Jumanne (Septemba 06) huenda nikawa sehemu ya kikosi kama Kocha atanipa nafasi, nipo tayari kupambana na kuisaidia timu kupata matokeo.” amesema Mshambuliaji huyo
Young Africans tayari imeshashuka dimbani mara mbili msimu huu, ikikusanya alama sita kwa ushindi wa 2-1 dhidi ya Polisi Tanzania na kisha Coastal Union iliyokubali kulala 2-0, Michezo yote ikipigwa Uwanja wa Sheikh Amri Abeid jijini Arusha.
Azam FC wao wamejikusanyia alama nne hadi sasa, baada ya kushinda dhidi ya Kagera Sugar 2-1, na baadae walilazimishwa sare ya 1-1 dhidi ya Geita Gold FC, Michezo yote ikichezwa Uwanja wa Azam Complex Chamazi.